Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam |
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa uamuzi wa kuwataka Mwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko kukaa rumande hadi Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa rufaa iliyofunguliwa kupinga uamuzi wa kufutiwa dhamana.
Rufaa hiyo ilifunguliwa na Wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala ambaye aliiomba mahakama hiyo kutoa amri ya kuwapa dhamana wateja wake.
Akisoma uamuzi huo mahakamani hapo leo Ijumaa Novemba 23, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri amesema, wakati rufaa hiyo ikiendelea Mahakama Kuu, washtakiwa hao wataendelea kukaa rumande hadi uamuzi wa mahakama utakapotolewa.
“Baada ya upande wa washtakiwa kufungua kesi ya rufaa ya kupinga uamuzi wa kuwafutia dhamana, washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu hadi uamuzi utakapotolewa,” amesema Hakimu Mashauri.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 6, mwaka huu itakapotajwa tena.