Elizabeth Joachim, Dar es salaam
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameiomba serikali kutafakari namna ya kupunguza msongamano wa watu mahabusu hasa katika Gereza la Segerea kwa kufanya upelelezi wa kesi zao.
Ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 15, jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa katika magereza hayo wako watu ambao hawastaili kukaa humo hasa kutokana na kesi zao.
“Kuna watu wako gerezani zaidi ya miaka minne hadi mitano, ukiuliza unaambiwa upelelezi haujakamilika mimi naona kama upelelezi haujakamilika basi waachiwe huru.
“Yaani hadi kule jela kuna mfungwa ametunga wimbo na si Mtanzania lakini ametunga wimbo wa Kiswahili akizungumzia namna magereza ya Tanzania yalivyojaa shida na kila ukienda mahakamani upelelezi unaendelea… hadi nilitamani ule wimbo ningeutoa kule gerezani watu wengine wausikie,” amesema Mbowe.
Aidha, amesema msongamano wa watu katika gereza hilo kumesababisha kuwapo na ugonjwa wa kujikuna hadi damu zinatoka unaosababishwa na ukosefu wa maji ya kuoga.
“Niombe sana kufutwa kwa kesi zisizo za lazima ili kupunguza msongamano wa watu katika magereza hayo na kufanya operesheni za kuweka dawa kwenye magodoro ili kuondoa ugonjwa huo wa kuwashwa walioubatiza jina la burudani,” amesema Mbowe.
Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema), amesema kuna changamoto nyingi alizokumbana nazo akiwa gereza la Segerea alikokaa kwa siku 104 msongamano wa wafungwa hasa wanawake ombaomba wenye watoto wadogo.
“Naiomba serikali kuangalia suhuhisho la jambo hili kwa kufuatilia kesi za wanawake hao.
“Nitoe rai kwa serikali mtu anapokuwa amekamatwa akiwa na kosa basi asomewe mashataka kama hatakutwa na kosa aachiwe huru na akikutwa na kosa afungwe ili kuepuka msongamano,” amesema.