27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

MBEYA KUJENGA BANDARI KAVU

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA

UONGOZI wa Mkoa wa Mbeya umejipanga kujenga bandari ya nchi kavu na kituo cha biashara kwa ajili ya kukuza uwekezaji.

Akizungumza baada ya kukagua eneo la ardhi lililotengwa na Halmashauri ya Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amosi Makalla, alisema Serikali imejipanga vizuri  kuufanya mkoa huo kukua kiuchumi.

Alisema Serikali imeendelea kutekeleza mkakati wa ukuzaji wa uchumi ambapo ekari 237 zimetengwa kwa ujenzi wa bandari ya nchi kavu na eneo jingine kubwa ambalo bado halijapimwa.

“Hivi sasa nchi ipo katika mpango wa ukuzaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda na kilimo, bandari hii ni moja ya fursa ya kiuchumi kwa mikoa ya nyanda za juu kusini,” alisema.

Alisema wafanyabiashara mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, hasa nchi za kusini mwa Afrika, hawatakuwa na ulazima tena wa kufunga safari kwenda Dar es Salaam kuchukua mzigo, badala yake shughuli zao zote zitakuwa zikiishia mkoani hapo.

Amewataka wananchi kuutunza mkoa huo na kuutumia kama fursa za kukuza uchumi, badala ya kuendekeza vitendo vya uvunjifu wa amani, ambavyo kwa kiasi kikubwa vimechangia kuuondoa kwenye ramani ya maendeleo.

Aliwataka vijana kujiepusha kufanya mambo yasiyo na tija, kama vile michezo ya pool mchana, unywaji wa pombe, uchezaji wa kamari na utumiaji wa dawa za kulevya.

“Vijana andamaneni kudai fursa, shamba, kufuga, ujasiriamali, badala ya kuendekeza vurugu zisizokuwa na msingi kwa taifa wala kwa jamii,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka wafanyabiashara kujipanga katika kutumia fursa ya kituo cha biashara kwa kuingiza biashara zenye tija na zitazokidhi ushindani wa soko la kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles