Theresia Gasper-Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Simba, Sven VandenBroeck, amesema watahakikisha wanaendeleza vipigo katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga, unaotarajiwa kuchezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba juzi waliendeleza ubabe mbele ya Azam baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2 katika uwanja huo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Sven alisema wamefurahi kupata pointi tatu muhimu dhidi ya Azam hivyo wataendelea kuonyesha makali yao keshokutwa na katika mechi nyinginezo.
“Kwa sasa tunajiandaa kukutana na Yanga Jumapili, hivyo mipango yetu ni kuendeleza ushindi kama tulivyopata dhidi ya Azam, naamini tutapambana na kuvuna pointi tatu muhimu,” alisema.
Alisema kwa muda huu uliobaki, ataendelea kuwanoa wachezaji wake ili wawe fiti na kupata kile anachohitaji.
Kocha huyo alisema anafahamu mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu hizo kuwa na upinzani, hivyo lolote linaweza kutokea.
Alisema watatumia makosa yatakayofanywa na wapinzani wao ili wapate mwanya wa kufunga mabao na kupata ushindi katika mchezo huo.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Simba na Yanga walitoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo uliochezwa katika dimba hilo.
Timu hizo zinakutana Simba wakiwa wanaongoza kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 68 baada ya kucheza mechi 26 wakishinda 22, sare mbili na kupoteza mara mbili.
Wapinzani wao, Yanga, wapo nafasi ya tatu na pointi 47 baada ya kucheza mechi 24, wakishinda 13, sare nane na kupoteza tatu.