MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
SIMBA imeandika rekodi mpya ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mchezo wa mwisho wa Kundi D uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kiungo Clatous Chama ndiye aliwawezesha Wekundu hao kutinga hatua hiyo, baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 90 akimalizia pasi ya John Bocco, likitanguliwa na lile la beki, Mohamed Hussein dakika ya 36.
Wageni kwa upande wao walijipatia bao pekee dakika ya 12 kupitia kwa Kasengu Kazadi.
Hii ni mara pili kwa Chama kuifungia Simba bao muhimu lililoipeleka timu hiyo hatua nyingine ya michuano hiyo.
Ikumbukwe kuwa, Mzambia huyo alifunga bao la tatu lililoiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia na kutinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo.
Ushindi wa juzi uliifanya Simba kufikisha pointi tisa na kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo, nyuma ya Al alhly ya Misri iliyomaliza na pointi 10, JS Soaura ikimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi nane, wakati AS Vita ikikwamia nafasi ya nne na pointi saba.
MTANZANIA imefanya tathmini ya kiufundi ya patashika ya juzi kati ya Simba na AS Vita.
Simba iliuanza mchezo huo kwa mpango kazi wa kumiliki mpira na kutengeneza mashambulizi, lakini kuwa makini kuhakikisha haiwapi nafasi wapinzani wao, uhuru ambao unaweza kuwaletea madhara.
AS Vita kwa upande wake iliuanza mchezo taratibu ikionekana kusoma nyendo za wapinzani wao, lakini iliongeza kasi kadiri muda ulivyozidi kusonga.
Wakongomani hao walionekana kudhamiria kutaka kumaliza mechi mapema kwa kupata mabao ya haraka.
Licha ya Simba kuanza vizuri kwa kucheza kwa kuelewana, wapinzani wao walikuwa makini kuziba nafasi zote ikiwemo eneo la kati ambalo wenyeji wao walikuwa wanalitumia kama kichocheo cha kutengeneza mashambulizi.
Uzoefu wa viungo kama Fabrice Ngoma, Wango Mbabu na Ernest Luzolo uliisadia AS Vita kutawala eneo la katikati, ambalo kwa Simba alikuwamo James Kotei, Mzamiru Yassin na Chama.
Baada ya kufanikiwa kutawala eneo hilo, viungo wa AS Vita walisababisha presha kwa mabeki wa Simba, kwa vile Mzamiru ambaye alikuwa amekabidhiwa majukumu ya kutibua mipango ya wageni kama ilivyo kwa Kotei kushindwa kutimiza kufanya yake.
Kudhibitiwa kwa Mzamiru kulisababisha timu kupoteza umiliki wa mpira na kujikuta wakifanya makosa mengi hasa kwenye eneo la ulinzi kutokana na wapinzani wao kuwabana, kiasi cha kushindwa kupiga pasi kutoka kwenye eneo lao.
Hatua hiyo ilichangia pia Chama kushindwa kufanya kazi yake sawasawa, kutokana na mipira kutomfikia, lakini hata alipoipata alishindwa kuipenyeza kwenye nafasi ili washambuliaji, Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere wafunge mabao.
Kupotea huko kwa Mzamiru kulisababisha Simba kuruhusu bao la mapema, baada ya Fabrice Ngoma kupiga pasi kwa Jean Marc Makusu ambaye naye aliutuma kwa Kazadi aliyeutendea haki kwa kuukwamisha wavuni.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems, aliuona udhaifu huo na kumwinua benchi Haruna Niyonzima kwa ajili ya kwenda kupasha.
Lakini kabla ya Niyonzima kuingia, Mzamiru alifanya tukio moja zuri baada ya kupenyeza pasi nzuri kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ iliyozaa bao la kusawazisha la Simba.
Baada ya kutoa pasi maridadi kwa Tshabalala, Aussems alisita kumtoa badala yake alimwacha hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika.
Kipindi cha pili Simba na mkakati wa kusaka bao la ushindi, ambapo ilitengeneza nafasi nyingi, kupitia kwa beki wa kulia, Zana Colibaly ambaye alikuwa katika kiwango bora katika mchezo huo.
Hata hivyo, utulivu mdogo wa Kagere uliikosesha Simba mabao.
Kwa ujumla, Simba ilikuwa na umiliki mkubwa wa mpira kipindi cha pili, hatua iliyolifanya lango la AS Vita kuwa katika kashkash mara kwa mara.
Wakati mchezo unaendelea, Aussems aligundua anahitaji mtu wa ziada mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na ndipo aliamua kumtoa Okwi ambaye hakuwa kwenye kiwango bora siku hiyo na kumwigiza Haruna Niyonzima.
Niyonzima alibadilsha hali ya mchezo mara hii Simba ilishambulia mfululizo na kwa kasi kubwa.
Uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kumiliki mpira wa Niyonzima, uliwafanya wageni kupata wakati mgumu wa kujilinda, lakini umaliziaji hafifu wa washambuliaji wa Simba uliwafanya wasidhurike.
Niyonzima alitengeneza nafasi za kufunga zaidi ya tano ambazo Kagere alishindwa kuzitumia kuuweka mpira kambani.
Kitendo hicho kilizidi kumuweka Aussems katika wakati mgumu, kwani muda ulikuwa unazidi kwenda, ndipo alipoamua kumtoa Mzamiru na kumwingiza Hassan Dilunga.
Hata hivyo, aligundua mambo bado magumu, hivyo akaamua kufanya mabadiliko mengine na kumtoa kiungo Kotei na kumwingiza kinda, Rashid Juma ili kuchochea mpango wa kusaka mabao.
Hatimaye dakika ya 90, Niyonzima aliunasa mpira, baada ya shambulizi la AS Vita langoni mwa Simba na kuwalamba chenga mabeki kadhaa kabla ya kupiga pasi kwa Bocco ambaye naye alimimina krosi safi ya chini chini iliyorukwa na Niyonzima na kumkuta Chama aliyeupiga mpira uliyekwenda kujaa wavuni kulia kwa kipa wa AS Vita, Nelson Lukong.
Mpaka hapo, ikafanikiwa kukata tiketi ya robo fainali na kuungana na timu nyingine saba ambazo ni Esperence ya Tunisia, Mamelodi Sun Downs ya Afrika Kusini, Wydad Casablanca ya Morocco, Haroya AC ya Guinea, TP Mazembe ya DRC na CS Constantine ya Algeria.