Na SHOMARI BINDA,
JESHI la polisi mkoani Mara, linamshikilia mtu mmoja aliyejifanya mwanasheria wa kujitegemea.
Mtu huyo alidaiwa kufanya utapeli wa mamilioni ya shilingi kwa watu mbalimbali aliowafuata  kuwasaidia katika masuala ya sheria.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Ramadhani Ng’anzi,alisema mtu huyo,  Joel Robert,alikamatwa Oktoba 13 katika Kijiji cha Kiterere wilayani Tarime baada ya  kumfuatilia.
Alisema mtu huyo alikuwa amekwisha kuwatapeli watu wengi ambao majina yao yanahifadhiwa.
Kamanda alisema mtu huyo amekuwa akiwatapeli watu kwa nyakati tofauti akijifanya ni wakili wa kujitegemea na kufuatilia masuala ya kesi kwenye vituo vya polisi na mahakama.
Ng’anzi alisema baada ya kupata taarifa za mtu huyo waliwatumia maaofisa wa upelelezi kumfuatilia na kumkamata na hivi sasa anaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
“Mtu huyu amefanya utapeli kwa muda mrefu kutokana na taarifa za watu waliotapeliwa ambao walizileta na sisi baada ya kumkamata tunaendelea kumuhoji na tukikamilisha upepelezi tutamfikisha mahakamani.
“Mtuhumiwa Joel anaonekana kuwa utapeli huu ameufanya kwa muda mrefu watu… wametapeliwa na majina yao tunayo lakini kutokana na masuala ya upelelezi tumeyahifadhi,”alisema Ng’anzi.
Kamanda  alitoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuwafichua watu au vikundi vinavyojihusisha na uhalifu ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aliwataka wananchi wanapotaka msaada wa sheria wafike kwenye ofisi zinazohusika na masuala hayo kupata msaada zaidi kuliko kudanganywa na watu wasiowafahamu na wanaojifanya wanatoa huduma ya sheria.