24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mbarawa aitaka TPA kufanya kazi kwa weledi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amewataka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao na kufanya kazi kwa weledi.

Amesema mamlaka hiyo imekabidhiwa dhamana kubwa na Serikali katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa weledi.

Profesa Mbarawa alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara kwenye mamlaka hiyo iliyolenga kuongea na uongozi pamoja na kukagua mradi wa upanuzi wa bandari pamoja na miradi mingine inayotekelezwa na mamlaka hiyo katika Jiji la  Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, Profesa Mbarawa aliikumbusha menejimenti ya TPA kwa kuwaeleza kuwa bandari ni uti wa mgongo katika uchumi wa nchi, hivyo jambo kubwa kwao ni kuhakikisha kuwa mapato yanaongezeka.

Alisema lengo hilo linaweza kutimia endapo kila mfanyakazi wa TPA akitimiza wajibu wake kwa kuzingatia mpango mkakati katika kutekeleza majukumu.

“Niliandaa mkataba wa utendaji hapo awali wa kukusanya shilingi trilioni moja na nitaendelea na utaratibu huo ambapo tutasaini  makubaliano ya makusanyo ili tuweze kwenda pamoja kiutendaji kuanzia bodi, mtendaji mkuu na watumishi wote,” alisema Profesa Mbarawa.

Aidha, alieleza kuwa ili kufikia lengo hilo la kukusanya kiasi hicho cha fedha ni lazima TPA wahakikishe wana rasilimali watu yenye uwezo, kuhakikisha wanapata maslahi kwa kuzingatia sheria pamoja na kuwekeza katika vifaa vya kisasa ili kuweza kuhimili ushindani wa soko.

Akiwasilisha taarifa, Mtendaji Mkuu wa TPA,  Eric Khamis, amemueleza Waziri Mbarawa  kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita TPA imefanikiwa kuongeza mapato kwa asilimia 38 jambo ambalo ni kiashiria kizuri katika uendeshaji wa bandari nchini.

Aliongeza kuwa kwa Agosti TPA ilifanikiwa kupakua tani mil. 1.7, ilikilinganishwa na malengo yaliyowekwa ya kuhudumia tani mil.1.4 kwa mwezi na kufanya TPA kutimiza malengo kwa asilimia 111.

Katika ziara hiyo, Prof. Mbarawa alitembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa upanuzi wa gati namba moja hadi saba ambao hadi sasa umefikia asilimia 99.

Mbali na hilo, pia Profesa Mbarawa alifanya ukaguzi katika kituo cha kupimia mafuta pamoja na sehemu ya kupokea mizigo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles