26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MBAO YAIKATA PUMZI SIMBA

Na MASYENENE DAMIAN-MWANZA

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wamepunguzwa kasi kwa mara nyingine katika harakati zao za kusaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kutoka sare ya mabao 2-2 na Mbao FC katika pambano lililofanyika kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Kabla ya mchezo huo, Simba ilicheza mechi tatu za ligi hiyo na kufanikiwa kuibuka na ushindi katika michezo miwili na kutoka sare mmoja.

Ilizindua kampeni zake kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, ikailazimisha sululu Azam FC kabla ya sare ya jana na Mbao FC.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi nane na kusalia katika nafasi ya pili na hivyo kushindwa kuishusha Mtibwa Sugar iliyoko kileleni ikiwa na pointi tisa, huku ikisubiri kuivaa Ruvu Shooting Jumapili hii.

Iliwachukua Simba dakika tatu tangu mpira kuanza  kufanya shambulizi, lakini mabeki wa Mbao waliondoa mpira kwenye eneo lao na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Dakika ya 11, Mbao ilijibu kwa kufanya shambulizi kali ambapo pande la Boniface Maganda lilimkuta Moses Shaaban ambaye alikunjuka mkwaju ambao uligonga mwamba wa juu wa Simba.

Dakika ya 16, Shiza Kichuya aliiandikia Simba bao la kuongoza kwa kichwa akiunganisha krosi ya Erasto Nyoni.

Baada ya bao hilo, Simba iliendelea kumiliki mpira, huku ikilisakama lango la Mbao na kufanikiwa kupata kona mbili katika dakika ya 19 lakini hazikuwa na faida.

Simba iliendelea kutawala hasa eneo la katikati ya uwanja, ambapo viungo wa timu hiyo, James Kotei na Mzamiru Yasini walionekana kucheza vema hivyo kuwapa tabu wapinzani wao.

Dakika ya 35, Mzamiru Yassin angeweza kuiandikia Simba bao la pili kama angekuwa makini, lakini mpira wake wa kichwa akiunganisha kona ya Nyoni ulipaa juu ya lango la Mbao.

Dakika ya 37, kocha wa Mbao, Etienne Ndayiragije, alifanya mabadiliko baada ya kumtoa Said Said na kumwingiza Herbert Lukindo.

Dakika ya 38, mwamuzi Athumani Lazi alimwonyesha kadi ya njano Yusuph Mgeta wa Mbao baada ya kumfanyia madhambi Kichuya, wakati dakika ya 45, Moses Shabani wa Mbao na  Jjuuko Murshid wa Simba walionyeshwa kadi za njano kutokana na mchezo usio wa kiungwana.

Kabla ya timu hizo kwenda mapumziko, kocha wa Simba, Joseph Omog, alifanya mabadiliko baada ya kumtoa Kichuya aliyeumia na kumwingiza Haruna Niyonzima.

Kipindi cha pili Mbao iliingia na mpango kazi wa kutaka kugomboa bao, ambapo dakika ya 46 ilifanikiwa kufunga bao la kusawazisha kupitia kwa Habib Kiyombo kwa mkwaju mkali wa chini chini uliomshinda kipa wa Simba Aishi Manula.

Bao hilo halikudumu kwa muda mrefu kwani dakika ya 50, kiungo James Kotei aliifungia Simba bao la pili baada ya kuunganisha kwa mguu mpira wa adhabu ndogo ulipigwa na  Nyoni.

Kuona hivyo, Mbao walifanya mabadiliko ambapo dakika 58 alitoka Moses Shabani na nafasi yake kuchukuliwa na Ndaki Robert.

Pia ilifanya mabadiliko mengine dakika ya 63, ambapo  alitoka Emmanuel Mvuyakule na kuingia  Ibrahim Njohole.

Dakika ya 69, Niyonzima alikuwa katika nafasi nzuri ya kuifungia Simba bao la tatu baada ya kupokea pasi ya Yassin lakini mkwaju wake ulipaa juu ya lango la Mbao.

Dakika ya 75, Omog alifanya mabadiliko mengine kwa upande wa Simba, alimtoa Nicholaus Gyan na kumwingiza Juma Luizio.

Mabadiliko ya Simba ni kama yaliisaidia Mbao kwani dakika ya 81 ilisawazisha kupitia kwa Boniface Maganga aliyepiga kwa ufundi mpira uliomshinda Manula na kujaa wavuni.

Bao hilo liliiongezea nguvu Mbao ambayo ilizidisha mashambulizi kwenye lango la Simba, lakini kikwazo kilikuwa kwa mabeki, Method Mwanjale na Salim Mbonde.

Dakika ya 88, Hussein Kasanga alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Mzamiru Yassin, hata hivyo mpira wa adhabu uliopigwa na Bocco uliishia mikononi mwa kipa Kelvin Igendelezi.

Dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2.

Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Jjuuko Murushid, Method Mwanjale, James Kotei, Mzamiru Yassin, Nicholaus Gyan/Juma Luizio, John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya/Haruna Niyonzima.

Mbao FC: Kelvin Igendelezi, Boniface Maganga, Abubakar Ngalema, Yussuph Mgeta, Yussuph Ndikumana, Sadala Lipangile, Raheem Njohole, Hussein Kassanga, Moses Shabani , Said Said na Habibu Kiyombo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles