Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
BONDIA kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Selemani Kidunda ‘Mtu Mbaya’, anatarajia kupanda ulingoni Desema 26, 2021 kuzichapa na Tshimanga Katompa raia wa DR Congo ambaye Oktoba, mwaka huu alimpiga Mtanzania Abdallah Pazi ‘’Dulla Mbabe kwa pointi jijini Dar es Salaam.
Kidunda anakutana na Katompa katika pambano ya kupigania mkanda wa WBF International, raundi 10 uzito wa kilo 76 kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini ambapo siku hiyo imepewa jina la Usiku wa Mabingwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Desemba 3, 2021 kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu Lugalo, Kidunda amesema amejipanga kuhakikisha anamlipia kisasi Dulla Mbabe.
“Kwanza namshukuru Mkuu wa Majeshi kwa kunipa kibali, najua jukumu nilipewa ni ngumu na mimi naweza nikalifanikisha, huyu bondia ashampiga ndugu yetu hapa Tanzania sasa hivi mmenipa mimi.
“Na mimi siku zote nasema nataka kuja kuwaonyesha radha Watanzania kwa huyu bondia hataweza kutoka, nguvu na sababu ya kumpiga tunayo, Watanzania wenzangu naomba ushurikiano wa kumtokomeza huyu mtu aliyempiga ndugu yetu.
“Nina uhakika tutampiga, tutampiga kwa kila njia, sababu nishajiandaa vya kutosha na ninaendelea na mazoezi chini ya makocha wangu, njooni muone udambwi udamwi,” ametamba Kidunda.
Kwa upande kocha wa Kidunda, Hassan Mzonge, amesema anatoa ujuzi wote kwa mabondia wake, anaamini Katompa hana pakutokea.
Katika rekodi, Katompa amecheza mapamno tisa ameshinda yote, matatu akishinda kwa K.O, wakati Kidunda tangu ameingia katika ngumi za kulipwa amecheza mapambano.
Kidunda tangu ameingia katika ulingo wa ngumi za kulipwa, amecheza michezo saba, ameshinda yote, sita kwa T.K.O, moja K.O, huku hili likiwa pambano lake ya kwanza la Kimataifa la kulipwa.
Muandaaji wa pambano hilo, Kapteni Selemeni Semunyu wa PeakTime Promotion, amesema tofauti na pambano hilo yatakuwepo mapambano mengine ikiwamo sita ya Kimataifa.
Kapteni Semunyu ameyataja mapambano hayo kuwa ni Ibrahim Class atazichapa na Israel Kamwamba(Malawi), Haruna Swanga(JWTZ) dhidi ya Daniel Matefu(Malawi), George Bonabucha(JWTZ) atapigana na Hassan Millanzi(Malawi), Ismail Galiatano(JWTZ) atachapana na Denis Mwale(Malawi) huku Grace Mwakamele akikutana na Ruth Chisale(Malawi), Hassan Ndonga na Yamikani Mkandawire(Malawi)
Ameyataja mapambano mengine ya utangulizi yanayowakutanisha Watanzania, Vigulo Shafii atacheza na Ally Kilongola, Idd Jumanne na Hamisi,Paul Magesta dhidi ya Oscar Richard,Paschal Manyota na Joseph Mchapeni, Najma Isike na Leila Yazidu.
Amesema mapambano yote yana baraka zote kutoka kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo naMnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Mathew Mkingule ambao wote wameahidi kutoa sapoti yao hadi mwisho.
Kapteni Semunyu amesema milango bado ipo wazi kwa yeyote anayependa kudhamini pambano hilo.
Kwa upande wa mmoja wa wadhamini wa mapambano hayo Afisa Mteule Daraja la Pili kutoka Suma JKT, amesema wameamua kutoa udhamini katika mchezo huo ili kuimarisha usalama siku hiyo ambapo welenga eneo la ulinzi.