Dk. Fredirick L Mashili, MD,PhD.
UKIFIKIRIA juu juu unaweza usiuone ukweli huu, kwamba mazoezi ni zaidi ya dawa. Leo tutajadili ukweli huu kwa kutumia shahidi zitokanazo na tafiti mbalimbali.
Mazoezi hutibu na kuzuia
Dawa nyingi huweza kutibu magonjwa lakini hazina uwezo wa kukukinga na magonjwa hayo. Lakini mazoezi huweza kutumika kama kinga na tiba ya magonjwa husika. Maana yake ni kwamba, wakati dawa hutumika tu baada ya kupata ugonjwa fulani, mazoezi huweza kutumika kabla na baada ya kupata ugonjwa huo kutokana na uwezo wake wa kuzuia na hata kuponya.
Chukulia dawa inayotumika kudhibiti sukari kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari inayoitwa metformin. Utafiti uliofanyika nchini Uingereza umeonesha kwamba mazoezi na lishe bora vinauwezo mkubwa zaidi wa kuzuia kutokea kwa ugonjwa wa kisukari ukilinganisha na uwezo wa dawa hiyo. Kutokana na hilo, hadi sasa ni mazoezi, lishe bora na mitindo mingine mizuri ya maisha ndiyo inashauriwa kutumika kama kinga ya ugonjwa wa kisukari. Hakuna dawa nyingine inayoshauriwa kutumika kama kinga. Dawa hutumika baada ya kupata ugonjwa huo ili kudhibiti kiwango cha sukari katika damu.
Mazoezi hutumika kuzuia na kudhibiti magonjwa zaidi ya ishirini
Wakati dawa moja hutumika kudhibiti au kutibu ugonjwa mmoja na mara chache magonjwa kadhaa, mazoezi hutumika kudhibiti magonjwa zaidi ya 20. Mazoezi hutumika kudhibiti ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya mayo na mapafu na magonjwa ya viungo na baadhi ya saratani. Hakuna dawa moja yenye uwezo huo. Tafiti na uzoefu vinaonesha kwamba watu wanaofanya mazoezi mara kwa mara huepuka kupata magonjwa takribani 20 ikiwamo baadhi ya saratani.
Tofauti na mazoezi hakuna dawa isiyokuwa na madhara ya pembeni – side effect
Daktari anapokuandikia dawa atakueleza madhara kidogo yatokanayo na utumiaji wa dawa hiyo. Mfano kusikia kichefuchefu, kutapika na hata kuvimba miguu kwa baadhi ya dawa. Haya huwa ni madhara kidogo lakini huweza kumfanya mtu akajisikia vibaya. Tofauti na muda na kuchoka mazoezi hayana madhara kama hayo. Chukulia baadhi ya dawa za kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu ambazo pia huweza kumfanya mwanamume kupungukiwa na nguvu za kiume. Endapo mtu angezuia au kudhibiti tatizo hilo kwa kufanya mazoezi angeweza kuepukana nalo. Hata hivyo, ikumbukwe kwamba, madhara haya huwa ni kidogo ukilinganisha na ya kutokutumia dawa hizo endapo daktari atashauri zitumike. Muhimu hapa ni kukwepa kufikia hapo kwa kujikinga na magonjwa hayo kwa kufanya mazoezi mara kwa mara.
Gharama ya mazoezi ni ndogo ukilinganisha na dawa
Tofauti na muda, baadhi ya mazoezi kama vile kutembea na kukimbia hayana gharama kabisa. Mazoezi mengine yanayohusisha kutumia vifaa maalumu yanahitaji kuwekeza mara moja tofauti na dawa zinazohitajika kila siku. Chukulia mtu anayeishi na ugonjwa wa kisukari na kupanda kwa shinikizo la damu anayetumia dawa za kudhibiti sukari na shinikizo la damu kwa wakati mmoja. Mtu huyu anatakiwa kutumia dawa hizo kila siku. Gharama yake ni kubwa mno. Lakini uwezekano wa kuwa amezuia matatizo hayo kwa kufanya mazoezi mara kwa mara ulikuwapo. Ziko tafiti za kiuchumi zilizofanyika na kuonyesha faida za kiuchumi za kufanya mazoezi mara kwa mara. Utastaajabu ukifuatilia matokeo ya tafitihizi pale utakapogundua kwamba kufanya mazoezi ni kuwekeza kifedha.
Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana naye kwa namba 0752255949, baruapepe, Fredirick@gmail.com. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org