30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mazito yamkabili mchekeshaji aliyeukwaa Urais Ukraine

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

AWALI, alifahamika kwa kipaji chake cha uchekeshaji lakini sasa rasmi Volodymyr Zelensky ndiye Rais wa Ukraine, akimwacha mbali mpinzani wake, Petro Poroshenko, katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni, Zelensky alizoa asilimia 73 ya kura zilizopigwa.

Si tu ushindi, pia Zelensky ameandika historia ya kuwa Rais wa kwanza kuingia Ikulu akiwa na tofauti kubwa ya kura dhidi ya mpinzani wake tangu nchi hiyo ilipopata uhuru miaka 30 iliyopita.

Pia, kasi yake kueleka katika ushindi huo imekuwa gumzo kwani baada ya kutangaza nia mapema mwaka huu, ilimchukua miezi miwili tu kushinda kwa asilimia 30 raundi ya kwanza ya uchaguzi huo, na kisha wiki tatu kutangazwa mshindi dhidi ya  Petro Poroshenko aliyetaka kurejea madarakani. 

Akiwa hana uzoefu wa masuala ya kisiasa, umaarufu wa ‘bwana mdogo’ huyo mwenye umri wa miaka 41 umetokana na uchekeshaji wake katika igizo lake la televisheni la ‘Servant of the People’ (Mtumishi wa Watu), ambalo lina wapenzi wengi katika Taifa hilo lenye watu milioni 45.

Kwa faida ya wengi, katika tamthilia hiyo, Zelensky ameigiza nafasi ya mwalimu aliyegombea na kushinda urais kwa lengo la kuwakaba koo viongozi ‘wapigaji’. Hivyo, igizo lake hilo limeakisi safari yake halisi ya Ikulu.

Huku akitumia mitandao ya kijamii kuwafikia wapiga kura wake, wengi wao wakiwa ni vijana, wapo waliolichukulia hilo kuwa ni udhaifu mkubwa wa Zelensky katika kuzungumza hoja za msingi.

Mmoja kati ya hao ni Profesa wa siasa katika Chuo Kikuu cha Kyiv-Mohyla Academy, Oleksiy Haran, alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha Al Jazeera, amesema “Watu walivutiwa na rais wa uongo waliomtazama kwenye ‘muvi’ yake, wakiamini ni ukweli. Ni suala la kisaikolojia. Zelensky anapozungumza, huwa ana makosa mengi.  Ndiyo maana upande wa timu yake ulikuwa ukiepuka mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Zelensky na waandishi wa habari au wataalamu.”

Ni kweli hiyo ya kukosa uzoefu inaweza kuwa hoja yenye mantiki lakini haitakuwa mara ya kwanza kwa wananchi wa Taifa hilo kumchagua mgombea nje ya ulingo wa siasa, mfano mzuri ukiwa ni pale bingwa wa zamani wa uzito wa juu, Vitali Klitschko, aliposhinda kuwa Meya wa Kyiv mwaka 2014.

Madai yaliyopingwa vikali na Zelensky aliyesema kukwepa midahalo na mahojiano ilikuwa moja kati ya mbinu zake za kushinda uchaguzi na tayari ameshapokea pongezi nyingi kutoka kwa mataifa mbalimbali, yakiwamo Marekani na Ufaransa.

Je, ni changamoto zipi zinazomkabili Zelensky kueleka safari yake ya miaka mitano Ikulu ya Ukraine? Kwa maana nyingi, yapi matarajio ya wachambuzi wa siasa na wananchi wa taifa hilo kwake?

Kibarua cha wazi kinachoweza kuonekana ni kuwathibitisha wakosoaji wake kuwa si kibaraka wa mfanyabiashara anayeshika nafasi ya tatu kwa utajiri nchini humo, Ihor Kolomoyskyi.

Kutokana na tuhuma za rushwa, akaunti za benki za Poroshenko zilitaifishwa mwaka 2016 zikiwa na zaidi ya Dola za Marekani bilioni 5.5 na ndipo alipokimbilia Israel.

Kwa kuwa hata tamthilia yake ya ‘Servant of the People’ ilikuwa ikirushwa na kituo cha televisheni kinachomilikiwa na bilionea huyo, basi kuna shaka kuwa Zelensky ni mtu wa karibu wa Kolomoyskyi.

Rais aliyemaliza muda wake, Poroshenko, ni mmoja kati ya wanaoamini hivyo, kwamba ushindi wa Zelensky ni kicheko ambaye hana uhusiano mzuri na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Kama hiyo haitoshi, inaaminika kuwa hata walinzi wa Zelensky ni wale waliokuwa wakifanya kazi na Kolomoisky, ikielezwa pia alimtumia hata mshahuri wa zamani wa tajiri huyo wakati wa kampeni. 

Hayo yanatajwa huku yakiwapo madai mengine kwamba magari mawili ya kifahari aliyokuwa akitumia Zelensky yanamilikiwa na watu wa karibu wa Kolomoisky, ingawa wawili hao wamekataa, wakisema uhusiano wao ni wa kibiashara tu na hauathiri maisha yao ya kisiasa. 

Licha ya Zelenskiy kukanusha kuwa kibaraka, wanaomtaja wanatilia shaka uwezekano wa wafanyabiashara wakubwa kurejesha nguvu yao katika uendeshaji wa Serikali kwa masilahi yao.

Mbali ya hilo, Zelenskiy akabaliwa na mtihani mzito wa kuyamaliza machafuko yanayoendelea Mashariki mwa Ukraine, ambayo yanachangiwa na vikundi vinavyoungwa mkono na Urusi, ikielezwa kuwa yameshagharimu maisha ya watu 13,000.

Tangu Urusi ilipolikalia eneo la Crimea mwaka 2014, Jeshi la Ukraine limekuwa likipambana kurejesha amani bila mafanikio. Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya Serikali ya Moscow kuzishikilia meli tatu za kijeshi za Ukraine. 

Tatizo ni kwamba mamlaka za Urusi hazijawahi kuamini kuwa Ukraine ni sehemu ya taifa lao na si nchi inayojitegemea, kama alivyowahi kusema Rais wa Urusi, Vladmir Putin, kuwa mataifa hayo ni kitu kimoja.

Ieleweke kuwa machoni mwa viongozi wa Urusi, Ukraine imekuwa ikitumiwa na mataifa ya Kibepari, ikiwamo Marekani. Utafiti uliowahi kufanywa na Kituo cha tafiti za kisaikolojia cha Levada, uliwahi kubaini kuwa asilimia 56 ya Warusi wanawachukia wenzao wa Ukraine.

Je, baada ya Poroshenko kuchemsha kwa kipindi chote cha uongozi wake, Zelensky ataweza? Katika hilo, mchambuzi wa siasa nchini Ukraine, Mykola Davydyuk, anasema: “Huenda Zelensky akatafuta mbinu za kidiplomasia na si kutumia jeshi.”

Kuonyesha ni kwa kiasi gani inaweza kuwa ngumu kwa Zelensky katika hilo la kumaliza uhasama uliopo kati ya mataifa hayo, tayari Urusi wameshatangaza kuwa watasitisha kupeleka mafuta na makaa ya mawe nchini Ukraine kuanzia Juni mosi, mwaka huu.

Urusi wanatangaza hatua hiyo huku Ukraine ikiwa wateja wakubwa wa makaa ya mawe kutoka kwa jirani zao hao, ikiagiza asilimia 23 ya bidhaa hiyo. Kando ya hilo, wakati uchaguzi uliomweka madarakani Zelensky ukiendelea, Jeshi la Ukraine lilitangaza kuwa vikundi vinavyoungwa mkono na Urusi vinaendeleza machafuko.

Ahadi ya Zelensky juu ya mgogoro huo ni kauli yake ya kusema huu ni wakati mwafaka kwa serikali yake itakayoanza kazi Juni 3, mwaka huu kuipeleka Ukraine katika karne ya 21.

Ziara yake nchini Ufaransa alikokwenda kukutana na Rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron, hata kabla ya kuingia madarakani, imewapa matumanini ‘watu’ wake, ikiwaamisha kuwa huenda ukawa mwanzo wa uhusiano mzuri na mataifa mengine kama Urusi.

Wakati huo huo, Zelensky anaingia Ikulu akitambua kuwa ana mzigo mzito wa kumaliza kero za kiuchumi ambazo ameachiwa na serikali zilizopita, ikiwamo aliyoing’oa madarakani ikiwa imekaa muhula mmoja.

Hadi leo hii, Ukraine imeendelea kuteswa na deni la mwaka 2014, walipokopa Dola za Marekani bilioni 17.5 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Mbaya zaidi kwa Zelensky, Mtafiti wa Fedha mjini Kiev, Oleksandr Parashchiy, anasema: 

“Miaka mitatu ijayo, Serikali ya Ukraine itakuwa na deni la Dola bilioni 20 na haifahamiki fedha hizo zitapatikana wapi. Anatakiwa kulifanyia kazi suala hilo.”

Naye mtaalamu wa deplomasia anayeishi Kiev, Andreas Umland, anasisitiza kuwa licha ya miaka 30 ya chaguzi, ikipitia mikononi mwa viongozi wenye utaalamu wa siasa na uchumi, bado Ukraine imeendelea kuwa nchi masikini zaidi barani Ulaya.

Hali mbaya kiuchumi inaungwa mkono na mchambuzi wa siasa za Ukraine, Melinda Haring, anayesema: “Wanachokitaka wananchi wa Ukraine ni maisha ya kawaida tu lakini nchi inakuwa masikini wakati (Rais) Poroshenko amejitajirisha. Ni wazi watu walitaka mtu asiye na makandokando na uhusiano na wanasiasa.” 

Zaidi ya hayo, mtihani mwingine alionao Rais huyo ni namna atakavyoweza kupata uungwaji mkono wa Bunge, ikiwa sehemu kubwa ya viti inakaliwa na wapambe wa rais aliyetangulia, Poroshenko.

“Haitakuwa rahisi kupata sapoti ya Bunge. Ni wazi atakuwa na Bunge lenye chuki (dhidi yake),” anasema mchambuzi wa siasa mwenye makazi yake mjini Kiev, Anatoliy Oktysuk.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles