20.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Muungano utukumbushe fikra za waasisi wetu

Na LEONARD MANG’OHA

WIKI hii nchi yetu imesherehekea miaka 55 ya kuzaliwa kwake tangu Chama cha Tanganyika African Union (Tanu), kilichokuwa kikitawala Tanganyika na Afro Shiraz Party kilichokuwa kikiongoza Zanzibar kuungana na kuwa nchi moja.

Miaka 55 inatimia wakati kukiwa na ombwe kubwa la kisiasa nchini kutokana na vilio kuhusu kubanwa kwa demokrasia, kunakofanywa na Serikali dhidi ya vyama vya upinzani.

Vilio vingi vinahusu kukosa uhuru wa kukusanyika, kuandamana na kufanya mikutano ya hadhara ambayo imepigwa marufuku na ile ya ndani ambayo pia mara nyingi imekuwa ikivurugwa.

Kutokana na hali hiyo hakuna tena kujiamini miongoni mwa vyama hivyo kutokana na vitisho na kufikishwa mahakamani kwa viongozi wake. Mathalani wakati huu viongozi wengi waandamizi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaburutwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kinyume cha utaratibu.

Wadau mbalimbali wanaelezea hali hiyo kama njia ya kuvikandamiza vyama vya upinzani kwa makusudi.

Tunapoadhimisha miaka 55 ni vema tukarejea nyuma na kutazama mawazo na fikra za waasisi wa muungano huu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Tukirejea maandiko ya Baba wa Taifa katika kitabu chake cha ‘Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania’, anaonyesha nia yake ya kutaka kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi. Tamaa hiyo ya Mwalimu Nyerere inatokana na kile alichokiita ubovu wa uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ndiyo uliofanya apendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi. 

“Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala CCM au ambacho kingekilazimisha Chama Cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao.

“Lakini bado sijakiona chama makini cha upinzani, wala dalili zozote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini, hili si jambo la kutarajia bila ya hofu na wasiwasi! 

“Wazalendo Watanzania hawana budi wapende kuona demokrasia halisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Hii ina sura mbili, Kwanza, ni lazima kurudisha tena uhuru na utaratibu wa kujadili masuala yote makubwa na kufikia uamuzi baada ya mjadala” inaeleza sehemu ya maandiko hayo.

Maneno ya Mwalimu katika kitabu hiki yanaonyesha ni kwa jinsi gani kama kiongozi wa chama na Taifa hakuwa na mawazo mgando ya kukumbatia chama chake tu hata pale alipoona kinaboronga, alifahamu wazi ili kuijenga CCM imara ni lazima kuwa na chama kingine chenye kutoa upinzani wa kweli kwa chama chake.

Zaidi ya miaka 25 sasa tangu Mwalimu alipoeleza hayo, lakini ni ukweli usiopingwa kuwa bado hakuna chama imara cha kukiondoa CCM madarakani. Nasema hivi kwa kuangalia hali ilivyo katika vyama vingi vya siasa vya upinzani nchini. Vyama vingi havina nguvu ya kisiasa kama ile ya CCM, kwa sababu havina mtaji mkubwa wa wanachama na hata nguvu ya kifedha ya kuweza kujiimarisha.

Vile vilivyojaribu kujitanua misuli yake vimejikuta katika migogoro ya ndani na kujikuta vinamaliza muda mwingi kupigania fito ndani ya vyama badala ya kuvijenga vyama vyao viweze kutoa upinzani wa kweli kwa CCM, huku baadhi ya vyama kama vile Chadema vimekumbwa na mkwamo wa kisiasa ambapo viongozi wake mara kwa mara wamejikuta matatani wanapofanya shughuli za kisiasa.

Mwalimu hakuwa mwoga wa changamoto bali alizitumia kama kipimo cha uongozi bora na alichukia uongozi wa kutumia vitisho bali wenye kutumia hoja zaidi katika kufanya maamuzi.

“Viongozi wetu hivi sasa wanaogopa kutumia nguvu za hoja ili kutoa maamuzi muhimu. Kwa sasa wanatumia hila zaidi kuliko hoja; vitisho kwao ni mbinu rahisi zaidi kuliko adha ya kutumia akili na kupata hoja safi ya kumjibu mpinzani katika mjadala. Viongozi hawa wakipewa nafasi watatumia hoja ya nguvu tu; na hawatakuwa na haja ya kutumia akili. 

“Kichini chini baadhi yao tayari wameanza kutumia hoja ya vitisho. Na kama tukiacha utamaduni wa woga ukazagaa tutakuwa tunakaribisha udikteta. Uhuru hauji wala haudumishwi ila kwa kuwa tayari kulipa gharama zake; na vitu vyote vyenye thamani kubwa gharama yake ni kubwa,”

Mwalimu alipendelea CCM iendelee kujenga utaratibu na utamaduni wa kuchambua masuaIa makubwa katika mijadala, na kufikia uamuzi baada ya uchambuzi na mijadala ya kidemokrasia na ya wazi wazi. Na wanachama wake kwa vitendo vyao lazima wapige vita utamaduni wa woga na fidhuli ya viongozi.

Kwa mtazamo wake kwa wakati huo Mwalimu aliamini kwamba demokrasia peke yake ambayo ingeendelea kuwa na maana kwa nchi hii wakati wanasubiri kupata mpinzani mzuri na makini nje ya CCM, ni demokrasia ndani ya CCM. Hapa aliwasihi wanachama wa CCM kukitazama upya chama chao na kuona jinsi ya kuongeza demokrasia ndani yake kwa manufaa ya Tanzania nzima.

Ni wazi kuwa CCM kama chama mama katika siasa za Taifa hili ambalo sasa linafikisha umri wa mtumishi wa umma aliye katika umri wa kustaafu, kinawajibika kuimarisha demokrasia nchini. Kinao wajibu wa kuvionesha njia vyama vingeni nini wanapaswa kufanya ili kufikia mafanikio ya kisiasa yenye kulenga maendeo kwa Taifa na si kuendelea kukaa madarakani bila kuwa na tija.

Naamini bado CCM haijakamilisha kazi hii ya kukuza demokrasia ya vyama vingi kwa sababu ni ukweli usiopingwa kuwa vyama vingi bado ni dhaifu kupambana na CCM. Kwa hiyo tunapoadhimisha miaka 55 ya muungano tuyakumbuke maono ya waasisi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,592FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles