NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa klabu ya KMC umefikia uamuzi wa kusitisha kibarua cha kocha Mganda Jackson Mayanja, kutokana na mwenendo mbovu wa kikosi chao tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mayanja ambaye aliwahi kuinoa Simba, aliingia mkataba wa mwaka mmoja kuinoa KMC, akichukua mikoba iliyoachwa na mtangulizi wake, Etienne Ndayiragije aliyetua Azam FC kabla ya kuteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars.
Alianza kuiongoza timu hiyo katika michuano ya Kombe la Kagame ilyofanyika nchini Rwanda, huku timu hiyo ikiishia hatua ya makundi.
Mayanja alishindwa kuipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kutolewa na AS Kigali ya Rwanda kwa kuchapwa mabao 2-1 nyumbani.
Kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar ,anakuwa wanne kuachishwa kazi tangu Ligi Kuu Bara ilipoanza kutimua vumbi Agosti mwaka huu.
Wengine ni Athumani Bilal aliyekuwa akiinioa Alliance, Fred Minziro aliyekuwa akiifundisha Singida United na Mwinyi Zahera aliyetupiwa virago na Yanga.
Hata hivyo, majina ya makocha Masoud Djuma raia wa Rwanda na Mcameroon, Joseph Omogo yanahusishwa na kikosi hicho kilichokuwa moto wa kuotea mbali msimu uliopita.
Akizungumza jana Dar es Salaam,Ofisa Habari wa KMC, Anwar Binde alisema kuwa wamekubaliana na Mayanja kuvunja mkataba huo kutokana na masharti yaliyowekwa.
“Tumekubaliana kuachana na Mayanja kutokana na mwenendo mbovu wa kikosi chetu, pande zote mbili zimeridhiana kuachana kwa amani, hivyo tunamtakia kila la kheri huo aendapo,”alisema Binde.