25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mayanja apeleka ombi TFF

Jackson MayanjaADAM MKWEPU NA THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM

KOCHA  Mkuu wa  timu ya Simba, Jackson Mayanja, ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania  (TFF)  kuwa na utaratibu wa kuwatumia waamuzi kutoka nje ya nchi kwenye mchezo dhidi ya Yanga, ili kupunguza  malalamiko kutoka  kwa mashabiki na wadau wa soka nchini.

Ombi hilo limekuja baada ya Simba kufungwa mabao 2-0 na Yanga, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Februari 20, Uwanja wa Taifa.

Kipigo hicho  kimeifanya  Simba kuwa nafasi ya tatu, ikiwa  na pointi 45 sawa  na timu ya Azam ambao wametofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Akizungumza na MTANZANIA, Mayanja alisema kuwa hatua hiyo inatokana na kiwango cha waamuzi nchini kuwa dhaifu, hivyo  kushindwa kumudu mchezo dhidi ya watani hao.

“Mchezo huu ni mkubwa sana, waamuzi wa hapa nchini wanashindwa  kuumudu, ni muhimu kwa wahusika kuona haja ya mwamuzi wa mchezo atoke nje ya nchi ili kuepusha malalamiko ya wadau pamoja na mashabiki.

“Kuna wakati waamuzi wanaamua kuwapa zawadi timu wanazozipenda kama kilichotokea  kwetu, ingawa sitapenda kulizungumzia jambo hili sana,” alisema Mayanja.

Mayanja aliongeza kuwa uamuzi wa kubahatisha haufai kwenye mchezo kama huo, ambao una hamasa kubwa kutoka kwa mashabiki wa soka nchini.

“Kama uamuzi ungekuwa wa haki Yanga isingetufunga, lakini kwa aina ile ya uamuzi ilikuwa kama vile alitoa zawadi kwa timu hiyo,” alisema Mayanja.

Hata hivyo, Mayanja alisema kuwa bado hajakata tamaa ya kupigania kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, licha ya kufanya vibaya dhidi ya mahasimu wao.

Kocha huyo alisema kuwa anatarajia kuzungumza na wachezaji wake ili kujipanga upya kwa michezo mingine inayowakabili  katika  Ligi.

“Tunatarajia kuanza mazoezi leo ili kuwajenga wachezaji wangu kisaikolojia na kuyafanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita  yasijirudie kwa mara nyingine,” alisema Mayanja.

Alisema kwa sasa wanakabiliwa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Singida United, utakaochezwa katikati ya wiki hii  ambapo watahakikisha wanapambana kuona wanafanya vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles