NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Simba, Jackson Mayanja, amemzuia mazoezini beki wake, Abdi Banda kwa madai kuwa hana taarifa za ujio wake mazoezini.
Banda alisimamishwa kwa muda kuitumikia timu hiyo baada ya kukaidi agizo la kocha huyo alipomtaka aingie uwanjani kuchukua nafasi ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ katika mchezo kati ya timu yake na Coastal Union, uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Machi 19 mwaka huu.
Mchezaji huyo pia anadaiwa kugomea kutumia vifaa vyenye nembo ya wadhamini wao, hivyo uongozi ulilazimika kumpa barua ya kumueleza makosa yake na kumtaka ajieleze pamoja na kumuomba radhi kocha wake.
Uongozi ulilazimika kumsamehe Banda baada ya kupitia barua hiyo na kuridhika, ambapo jana alitakiwa kuanza mazoezi rasmi Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini.
Habari zilizoifikia MTANZANIA jana zilisema kuwa baada ya mchezaji huyo kufika uwanjani hapo, kocha Mayanja alimzuia getini na kumwambia kuwa hana taarifa za ujio wake.
“Kocha amemzuia kuingia kwa madai kuwa uongozi haujampa taarifa zozote kuhusu ujio wa mchezaji huyo, hivyo hawezi kumruhusu hadi apate taarifa,” alisema.
Kwa upande wake, Banda alikiri kuzuiwa na kudai Mayanja alimueleza hatambui uwepo wake hadi atakapotaarifiwa na uongozi.
“Nimefika hapa getini kocha amenizuia kuingia, anasema hana taarifa za ujio wangu, bado niko hapa sijui la kufanya lakini nataka kuondoka zangu,” alisema.
Alieleza, yeye alisamehewa na alitakiwa aanze mazoezi lakini anashangaa kuzuiliwa.
Gazeti hili lilipomtafuta Meneja wa klabu hiyo, Abbas Ally kuzungumzia sakata hilo, alisema Banda ameshamaliza adhabu yake na ameanza mazoezi.
“Taarifa za kuzuiliwa mazoezini hizo hatujazipata, lakini tunachofahamu kuwa Banda amemaliza adhabu yake na leo (jana) ameanza mazoezi,” alisema