NA MWANDISHI WETU
LICHA ya utamaduni wa Waswahili kuonekana kupungua kwa kiasi kikubwa, Tamasha la Kimataifa la Nchi za Jahazi (ZIFF) limekuwa mstari wa mbele kuendeleza tamaduni hizo ili zisipotee kabisa hasa katika maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki.
Mashindano ya Utamaduni wa Swahili ni moja kati ya matukio makubwa yanayoitambulisha ZIFF kitaifa na kimataifa kwa kuwa uhudhuriwa na watu wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Juzi kulifanyika mashindano ya Ngalawa hasa katika Pwani ya Bagamoyo ambapo ngalawa yenye nembo za Maximalipo iliyokuwa na waendeshaji 10 iliibuka mshindi wa jumla kati ya ngalawa 10 zilizoshindanishwa katika fukwe za bahari huko Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Maximalipo ilivunja ubabe wa ComNet iliyokuwa ikishinda kila mwaka katika mashindano kama hayo, hata hivyo washindi watatu wa shindano hilo ambao ni Maximalipo walioshika namba moja, wapili ni ComNet na wa tatu ni ComNet tena kwa pamoja wataungana na washindi watakaopatikana katika fukwe za bahari maeneo ya Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano ya fainali yatakayofanyika visiwani Zanzibar wakati wa Tamasha la ZIFF.
Mratibu wa shindano hilo, Omary Madongwa, baada ya kutangaza washindi alisema shindano la Dar es Salaam litafanyika katika fukwe za Msasani Beach na kisha washindi wake watajumuishwa katika mashindano ya mwisho yatakayofanyika visiwani Zanzibar wakati wa maadhimisho ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF).
Ili kuendeleza harakati hizo za tamaduni za Swahili, mashindano hayo ya Ngalawa kwa mwakani yanatarajiwa kufanyika katika mikoa mingi zaidi nchini badala ya Pwani na Dar es Salaam, Bagamoyo pekee.
Mikoa inayotarajiwa kuongezwa katika mashindano ya mwakani ni pamoja na Tanga na Mtwara huku kampuni zaidi za kibiashara zikiombwa kudhamini mashindano hayo.