NA CHRISTOPHER MSEKENA
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, juzi alizindua mfumo mpya wa usambazaji kazi za sanaa unaoitwa Max Burudani unaotarajiwa kuwa mkombozi wa wasanii wa muziki na filamu.
Uzinduzi huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Kisenga, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wasanii wa muziki na filamu waliokuwa na furaha kushuhudia mfumo wa Max Burudani.
Mfumo huo uliojielekeza zaidi katika sekta ya usambazaji, umebeba matarajio ya wasanii wengi waliokatishwa tamaa na mifumo ya kinyonyaji iliyofanya jasho lao wengi kupotea bure huku ikitoa faida kwa wezi wa kazi za sanaa.
Max Burudani ni mfumo wenye mawakala zaidi ya 16,000 nchi nzima ambapo unamuunganisha msanii na mlaji wa kazi za sanaa ambaye ni wewe shabiki. Mfumo huo umetengemaa tayari kuwahudumia mashabiki wa sanaa.
Nasema hivyo kwa sababu kampuni inayomiliki huo mfumo tayari inahusika kuihudumia jamii katika ulipaji wa bili mbalimbali kama za umeme, maji, ving’amuzi, kodi nk, lakini hivi sasa umewageukia wasanii ili kuwapa faida ya kazi yao ya sanaa.
Inafahamika tasnia ya filamu ilikwama wapi licha ya wasanii wake kuzalisha filamu katika mazingira ya shida, wamekuwa wakikutana na changamoto katika suala zima la usambazaji, kwa kiasi kikubwa hakukuwa na wawekezaji wenye dhamira ya dhati ya kuwanufaisha wasanii.
Hali hiyo ilipelekea anguko la soko la filamu kwani ilifika kipindi kama filamu yako ina ujumbe mzuri lakini ndani yake hakuna staa aliyecheza, basi msambazaji hapokei filamu yako hiyo, hivyo nayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa soko la filamu.
Lakini pia wasanii wa muziki waliacha kutoa albamu tatizo likiwa ni hilo hilo la kukosekana wasambazaji. Msanii wa muziki aliona bora atoe singo moja moja kuliko kutoa albamu yenye nyimbo 10, ambazo amegharamia kuziandaa kisha anaiuza kwa bei ya hasara.
Kwa masaibu hayo, Max Burudani imebeba matumaini mapya ya wasanii, hivi sasa wanatarajia kuanza kunufaika na kazi zao za sanaa, wale wa muziki watauza albamu zao na wanaofanya filamu soko la uhakika limepatikana ambalo linazingatia uwazi na ushirikiano kati ya msanii, shabiki na wawekezaji wenyewe.
Bila shaka wawekezaji wengine wataanza kumiminika kuwekeza kwenye masoko ya sanaa, kwani muziki na filamu ni bidhaa zenye uhitaji mkubwa usiokoma.