HARARE, Zimbabwe
MAWAZIRI wawili wa zamani wa Zimbabwe wamefikishwa mahakamani, wakishutumiwa kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa walipokuwa madarakani.
Samuel Undenge ambaye alikua Waziri wa Nishati anatuhumiwa kutumia Dola 12,000 kwa kampuni ambayo haikufanya kazi.
Kwa upande wa wake, Walter Mzembi, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wakati wa utawala wa Robert Mugabe aliyeondolewa madarakani mwezi Novemba, anatuhumiwa kuchangia baadhi ya mali za televisheni ya Taifa kwa kanisa moja nchini humo bila ya idhini ya Serikali.
Hata hivyo, wote wamekana mashitaka hayo na kesi zao zitaanza kusiklizwa tena baadaye mwezi huu.
Rais mpya, Emmerson Mnangagwa, ameapa kupambana na rushwa aliyosema imedumu kwa kipindi chote cha utawala wa Mugabe.
Lakini wakosoaji wanasema watu wanaokamatwa na kufikishwa mahakamani ni wale tu wanaohoji namna Mnangagwa alivyoingia madarakani.