25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MAWAKILI WATANGAZA MGOMO NCHI MZIMA

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

BARAZA la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), limewataka wanachama wake wote nchi nzima kususia kuhudhuria mahakamani kufanya kazi za uwakili na katika mabaraza ya aina zote Agosti 29 na 30, mwaka huu.

Hatua hiyo imefikiwa kwa lengo la kuwaunga mkono mawakili wa Kampuni ya IMMMA Advocates, kupinga ofisi zao zilizopo Upanga, jijini Dar es Salaam kulipuliwa kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.

Juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa IMMMA Advocates, Sadoc Magai, aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika tukio hilo walielezwa na polisi kuwa walikuta madumu yanayodaiwa kuwa petroli ingawa hawakutaja idadi yake.

Magai alisema alipigiwa simu na kufika eneo la tukio juzi saa 11 alfajiri. “Saa 11 asubuhi tulikuja, tukakuta polisi wapo tayari hapa. Majirani wanasema tukio lilitokea saa 7 usiku.

“Jengo limekuwa ‘damaged’ (limeharibiwa), hatujui sababu, hatujui nini kimetokea, huko ndani kuta zimevunjika, milango ambayo ‘partition’ yake (imegawanywa) ni vioo imebomoka,” alisema.

Kwa mujibu wa Magai, polisi pia waliwaarifu kuwa walinzi wao wawili wa Kampuni ya Knight Support waliokuwa wanalinda ofisi hizo siku ya tukio, nao walikutwa wametupwa eneo la Kawe wakiwa hawajitambui, mithili ya watu walioleweshwa dawa.

MAAZIMIO YA TLS

Akisoma maazimio ya baraza hilo Dar es Salaam jana, Rais wa TLS, Tundu Lissu, alisema kama mawakili hawako salama maana yake uwezo wa kuwawakilisha wateja wao hautakuwapo.

“Baraza la Uongozi limefanya kikao cha dharura Agosti 26, mwaka huu kujadili shambulio la mabomu dhidi ya ofisi za IMMMA Advocates.

“Katika kikao hicho, baraza limeazimia wanachama wote wa TLS nchi nzima kususia kuhudhuria mahakamani na  katika mabaraza ya aina zote  siku ya Jumanne na Jumatano ,”alisema Lissu.

Alisema ishara ya kutokubaliana na hilo, ni wazi wateja wao wataathirika na hata Mahakama hazitafanya kazi, lakini wameamua kufanya hivyo kwa sababu hawako salama.

“Tukiruhusu huu utaratibu wa kutega mabomu kwenye ofisi za mawakili, kesho watatega kwenye ofisi za waandishi wa habari na kwengineko…tunataka wananchi waelewe hili si jambo dogo…ni vyema tupate shida wote.

“Wakati nilipochaguliwa kuwa Rais wa TLS, nilisema shambulio dhidi ya wakili mmoja linatakiwa kuwa shambulio dhidi ya mawakili wote. ‘Solidarity’…akiumizwa mmoja tumeumizwa wote,” alisema.

Kutokana na hilo, alisema watamwandikia barua Kaimu Jaji Mkuu, kumweleza mawakili wao hawatakwenda mahakamani siku ya kesho na kesho kutwa.

Pia alisema baraza la uongozi linafanya utaratibu wa kuonana na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa ili kuzungumzia vitendo vya kushambuliwa kwa mawakili wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kisheria.

“Baraza litafanya jitihada za haraka kukutana na Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS)  na Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania ili kujadiliana juu ya suala hili na usalama wa mawakili wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kitaaluma,”alisema.

Alisema baraza hilo, pia limevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutumia mamlaka vilivyonavyo vya kiupelelezi kuhakikisha shambulio la mabomu dhidi ya ofisi hizo za mawakili, linachunguzwa na wahusika kuchukuliwa hatua.

“Baraza la uongozi linavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwahakikishia ulinzi wa kutosha mawakili wa IMMMA Advocates dhidi ya vitisho au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wao au kuwazuia kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kitaaluma.

“Pia Baraza linawataka wananchi kuhakikisha kwamba wanalinda usalama, uhuru na heshima ya wanasheria na mawakili nchini kwetu ili kuwawezesha kutekeleza wajibu wao wa kitaaluma wa kulinda utawala wa sheria na haki za binadamu,”alisema.

Alisema pamoja na kwamba ni mapema kufahamu mhusika, baraza linalaani kwa sababu kinaingilia uhuru wa wanasheria na kuhatarisha uhuru wa mahakama na utawala wa sheria kwa ujumla.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema kushambulia ofisi za mawakili kwa mabomu ni wazi kuwa kitendo hicho kina lengo la kuwazuia kutekeleza wajibu wao kama wanasheria.

“Kitendo cha kushambulia ofisi za mawakili kina lengo la kuwatisha mawakili hao wasiweze kutekeleza wajibu wao kama wanasheria na mawakili kwa kuwatia hofu ya kuwadhuru kimwili au kuwapotezea maisha yao.

MIKATABA YA KIMATAIFA

Lissu, alisema kitendo cha kushambulia ofisi hizo za mawakili, kinakiuka sheria za nchi na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

“Ibara ya 16 ya Kanuni za Msingi za Umoja wa Mataifa juu ya wajibu wa wanasheria za mwaka 1990 (UN Basic Principles on the Tole of Lawyers 1990) au ‘The Havana Principles’, inazitaka serikali za nchi wanachama kuhakikisha wanasheria wana uwezo wa kutekeleza majukumu yao bila vitisho.

“Ibara ya 17 ya kanuni hizo inasema pale ambapo usalama wa wanasheria unatishwa kwa sababu ya wao kutekeleza wajibu wao, basi watapatiwa ulinzi wa kutosheleza na mamkala.

“Ibara ya 8 ya Viwango vya Uhuru wa Taaluma ya Kisheria vilivyowekwa na Chama cha Mawakili Duniani (IBA) vya 1990, inatamka ; hakuna mwanasheria atakayechukuliwa au kutishiwa kuchukulia hatua zozote za kijinai, madai, kiutawala, kiuchumi.

“Au adhabu nyinginezo au kusumbuliwa kwa sababu ya yeye kumshauri au kumwakilisha mteja yeyote kwa mujibu wa sheria,”alisema.

Kutokana na hilo, alisema kilichofanyika katika ofisi hizo ni kitendo cha kigaidi kwa mujibu wa kifungu cha 4(3) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi, 2002.

WATEJA

Lissu alisema ofisi hiyo ya IMMMA, wanawakilisha Kampuni ya Madini ya Acacia Mining PLC ya Uingereza ambayo ina mgogoro mkubwa unaoendelea baina yake na Serikali.

Pia mawakili hao wanamwakilisha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad katika mashauri yanayohusu mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho.

“Mawakili wa IMMMA pia ni sehemu ya timu ya mawakili wanaomwakilisha Rais wa TLS katika kesi kadhaa za jinai.

“Wakili Fatma Karume wa IMMMA Advocates amefungua mashauri ya madai dhidi ya askari wa Jeshi la Polisi aliyemshambulia wakati akiwa anatekeleza wajibu wake kama wakili wa Rais wa TLS.

“Hata hivyo, sheria zinazohusika zimeweka wazi katika kutekeleza wajibu wao wa kitaaluma, wanasheria wasitambulishwe na mamlaka za nchi au na wananchi kutokana na masilahi ya wateja wao katika mashauri,” alisema.

Lissu alisema inawezekana baadhi ya kazi ambazo wamekuwa wakizifanya mawakili wa IMMMA Advocates siku za karibuni zinaweza kuwa sababu.

Akizungumzia shambulio hilo, alisema baraza limepata taarifa  usiku wa kuamkia Agosti 26, mwaka huu, kikundi cha watu kadhaa wakiwa wamevalia sare zinazodhaniwa kuwa za polisi, wakiwa na silaha za moto, kiliwateka nyara walinzi binafsi wa ofisi hizo.

“Watu hao wakiwa katika magari mawili walidai wanafukuza majambazi; wakawaambia wale walinzi  wafungue geti kwa sababu kuna jambazi mmoja karuka ukuta na mwingine wamemkata na kumfunga pinga (wanamwonyesha alifungwa pingu akiwa katika gari).

“Sasa unafikiri security wakishaona polisi wangefanyeje na wana bunduki, kwa hiyo wakawafungulia wakawadunga sindano na kulewa.

“Walivyoingia ndani ya ofisi za mawakili hao walitega milipuko na madumu manne ya mafuta ya petrol katika maeneo kadhaa ya jingo hilo.

“Muda mfupi baadaye, milipuko hiyo ililipuka na kusababisha uharibifu mkubwa wa jengo la ofisi za IMMMA pamoja na majengo ya jirani.

“Baadaye walinzi wakaokotwa mahali fulani huko Kawe na sasa nasikia wako Muhimbili, nani alifanya haya? Hatufahamu. Sasa vyombo vya ulinzi wao watuambie nani alifanya jambo hili mbaya,”alisema.

Kwa upande wake, Rais wa TLS  Zanzibar, Omar Said Shabani alisema matukio hayo yakinyamaziwa itafika hatua mawakili watauawa na kupotezwa.

“Nami nimekuja kupinga na kulaani hili…ofisi yangu ilishawahi kupata dhahma hii lakini Jeshi la Polisi halijawahi kuja na ripoti yoyote hadi leo,”alisema Shabani.

Alipotafutwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema bado uchunguzi unaendelea kuhusu suala hilo na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baada ya uchunguzi kukamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles