29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mawakili waandamana kudai haki

Mawakili wa kujitegemea wakiandamana kuelekea Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kupinga vitendo vya ukiukwaji wa sheria za nchi na kazi za uwakili unaodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi.
Mawakili wa kujitegemea wakiandamana kuelekea Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kupinga vitendo vya ukiukwaji wa sheria za nchi na kazi za uwakili unaodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi.

Na ELIYA MBONEA – ARUSHA

MAWAKILI wa kujitegema zaidi ya 100 mkoani Arusha, jana waliandamana kwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, kulaani kile walichokiita ukandamizwaji wa sheria za nchi na kazi ya uwakili unaofanywa na polisi.

Wanasheria hao wanalaani kitendo cha wakili mwenzao, Shilinde Ngalula, kukamatwa, kufungwa pingu na kufunguliwa mashtaka akiwa kazini Loliondo wilayani Ngorogoro.

Mawakili hao walitembea zaidi ya hatua 400 kabla ya kuzingirwa na polisi ambao waliwataka kuunda kamati ya watu wachache kwenda kuzungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo.

Uamuzi wa kufanya maandamano hayo, ulipitishwa jana mjini hapa baada ya mawakili hao kufanya kikao cha pamoja viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Awali, mawakili hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Modest Akida, pia walikubaliana kutoendelea na kesi za wateja wao waliokuwa mahakamani.

Akizungumzia maandamano hayo, Akida alisema yalilenga kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi wilayani Ngorongoro, kumkamata na kumfungulia mashitaka Wakili Ngalula.

Wakiwa tayari wameandamana umbali wa takribani hatua 400 kutoka mahakamani hapo, vikosi vya askari polisi waliovalia kiraia na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa ndani ya magari mawili, waliwazunguka na kuwaamuru kusimama.

Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Thomas Mareko, aliwataka wanasheria hao kufuata sheria katika kudai na kuwasilisha malalamiko yao.

“Nyinyi ni wanasheria, mpaka hapa tayari mmeshaandamana kinyume cha sheria za nchi, nawaomba chagueni wawakilishi nitawasindikiza mnakokwenda na wengine rudini mkaendelee na majukumu yenu,” alisema Mareko.

Baada ya maandamano hayo kuzuiwa, mawakili hao waliwachagua wawakilishi waliokwenda kuwasilisha malalamiko yao kwa Kamanda Mkumbo na wengine walirudi katika viwanja vya mahakama kusubiri taarifa.

Awali, akizungumza katika viwanja hivyo, Wakili George Njooka alisema mawakili nchini wameanza kudharauliwa na vyombo vya dola.

“Hawa watu walianza na vyombo vya habari, wakaenda kwa wanasiasa na sasa wamekuja kwa mawakili, nawaomba tuanzie hapa twende kwa RPC atuambie haya maelekezo tunayoambiwa yanatoka juu, yanatoka kwa nani,” alisema Wakili Njooka.

Wakili Qamara Peter aliwakumbusha mawakili wenzake kuwa haki siku zote haiombwi bali inadaiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles