25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mawakili wa Mansour wawasilisha hati ya kuomba dhamana

Aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himid
Aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himid

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MAWAKILI wanaomtetea waziri wa zamani wa Zanzibar, Mansour Yussuf Himid, wamewasilisha rasmi ombi la dhamana chini ya hati ya dharura (certificate of urgency) katika Mahakama Kuu ya Zanzibar ambayo ndiyo yenye uwezo wa kutoa dhamana kwa aina ya makosa aliyoshtakiwa nayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, ilieleza kuwa mawakili hao, Fatma Karume, Gasper Nyika na Tundu Lissu wanaomtetea Mansour waliwasilisha hati hiyo mahakamani hapo jana.

Jussa alisema baada ya kuwasilisha hati hiyo, mawakili hao walikwenda katika gereza la Kiinua Miguu lililoko Kilimani mjini Unguja kwa lengo la kumuona mteja wao pamoja na kumpa taarifa juu ya hatua hiyo.

“Baada ya kuwasilisha hati ya dharura katika Mahakama Kuu Zanzibar, mawakili walikwenda katika gereza la Kiinua Miguu ambalo Mansour amewekwa mahabusu ili waweze kuzungumza naye na kumpa taarifa juu ya hatua wanazochukua ikiwamo ya kuwasilisha hati hiyo ya dharura,” ilieleza taarifa ya Jussa.

Alisema Mansour aliwaambia mawakili hao hali yake ni nzuri na kuwaomba Wazanzibari wamuombee dua tu kwa Mwenyezi Mungu ampe subira katika kipindi hiki.

“Leo (jana) tulipigiwa simu na Ofisi kadhaa za kibalozi za nchi za nje zikitaka kujua kinachoendelea na tumewapa taarifa kwa ukamilifu,” iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo, Jussa alieleza kuwa mama mzazi wa Mansour, Fatma Mohamed Jinja, pamoja na mkewe, Asha Karume wameomba wafikishiwe salamu zao kupitia mtandao wa jamii kwa watu wote waliosimama nao katika kipindi hiki kigumu na kwa jinsi walivyoonesha mapenzi na hisia zao kwa Mansour.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa, wanaamini haki itatendeka na atashinda katika kesi hiyo.

Kutokana na hali hiyo aliwataka Wazanzibari kuwa watulivu na hali ya amani wakati kadhia hiyo inazidi kufuatiliwa.

Mansour anatuhumiwa kutenda makosa matatu likiwamo la kukutwa na silaha pamoja na risasi kinyume cha sheria.

Mansour alikamatwa na polisi Agosti 2, mwaka huu saa 07:18 mchana katika eneo la Chukwani Mjini Unguja ambapo baada ya kupekuliwa alikutwa na bastola ya Baretta yenye namba F76172W.

Kitendo hicho kinakwenda kinyume na sheria namba 6(3) na 34(1)(2) cha sheria ya mwaka 1991 sura ya 223 ya sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kosa la pili analoshitakiwa nalo Mansour ni pamoja na kupatikana na risasi za moto 295 za bastola jambo ambalo pia ni kosa kisheria.

Alifikishwa katika mahakama ya Vuga Agosti 5 mwaka huu na kusomewa mashitaka yanayomkabili lakini akarejeshwa rumande baada ya mahakama kudai kosa linalomkabili la kukutwa na silaha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 18, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles