Na Samwel Mwanga, Maswa
MAMLAKA ya Maji na Usafi na Mazingira mjini Maswa(MAUWASA) iliyoko katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imewataka wananchi kujisalimisha kwenye ofisi za mamlaka hiyo ili waweze kuunganishiwa maji kiuhalali na kuacha kuchepusha maji kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
MAUWASA wameendelea na ukaguzi wa miundombinu ya maji inayohujumiwa na wananchi wasio waaminifu na kusababisha mamlaka hiyo kupata hasara.
Zoezi hilo limekuwa endelevu kwa wateja wa maeneo yote yanayohudumiwa na mamlaka hiyo na kufanikiwa kugundua maeneo ya baadhi ya watu mbalimbali wakiwa wanaunganisha maji kwa njia wa wizi.
Matukio ya wizi wa maji yameendelea kuvumbuliwa kwa kasi kubwa ambapo jitihada za Mamlaka zimefanikiwa kuwakamata watu mbalimbali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Raphael Mwita amesema kuwa wamemkamata, Clement Masalu mkazi wa kijiji Dodoma wilayani humo ambaye amehujumu miundo mbinu ya maji ya Mauwasa na kujitengenezea bwawa na kuuza maji bila utaratibu na kuipatia hasara mamlaka hiyo.
Amesema waliweza kugundua wizi huo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kijijini hapo na ndipo walipotumia jeshi la polisi kumkamata.
“Alichokuwa anakifanya alikwenda kwenye bomba la maji akalikata kisha akaunga mipira miwili ambayo imekuwa ikipeleka maji kwenye bwawa hilo ambalo amelichimba hivyo kuwauzia wananchi maji kwa ndoo moja Sh 100 na mifugo kunyweshea Sh 30,000 kwa mwezi,”amesema Mwita.
Amesema walibaini kuwa bwawa hilo lina urefu wa mita 35, upana mita 11 na kina cha mita 1.2 na lina uwezo wa kujaza maji lita 462,000.
Nae Meneja Biashara wa Mauwasa, Boniface Kasinde amesema wameweza kupata taarifa ya wizi wa maji na wamechunguza na kugundua kuwa wizi mkubwa unaofanywa naadhi ya watu ni kwa njia ya kujiunganishia maji nyuma ya mita ya maji.
“Kujiunganishia maji nyuma ya mita ni kosa kisheria unakuwa unahujumu Mamlaka na utakapobainika sheria itachukua mkondo wake maana unakuta mtu amesitishiwa huduma lakini ndani ya nyumba yake kuna maji.
“Ni kosa kisheria na mteja anaunganisha maji nyuma ya mita anakuwa amefanya hujuma na hasara kwa serikali na makosa haya yanapelekea kulipa faini au kufunguliwa kesi na kupelekwa mahakamani na atalipa gharama zote za uharibifu uliofanywa,” amesema Kasinde.
Kasinde ameongeza kuwa miundo mbinu hii ni ya muda mrefu na kipindi cha nyuma mita za maji zilikuwa zinafungwa kwa ndani na sasa tumeamua mita zote kuzifunga nje ya uzio wa nyumba.
Mauwasa imeendelea kuwataka wananchi kuacha kuhujumu miundo mbinu ya maji kwani utakapokamatwa sheria itachukua mkondo wake na hakutakuwa na huruma kwa mtu yoyote na faini ni kuanzia Sh 500,000 hadi milioni 10 au kifungo kisichopungua miezi sita hadi miaka miwili jela au vyote viwili kwa pamoja.
Wateja wa Mauwasa wameombwa kuacha kuchepusha maji na zaidi wajisalimishe kwenye mamlaka ili kuweza kupata huduma ya maji kwa uhalali na kuacha kuhujumu miundi mbinu ya mamlaka.