WATU waliojihami kwa silaha nzito, wameua watu 29 katika mashambulizi pacha yaliyotokea usiku wa kuamkia jana katika maeneo ya pwani ya Kenya.
Mashambulizi hayo mawili ni sehemu ya mlolongo wa mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab.
Wanamgambo hao wa Kiislamu wa Somalia wameapa kuendelea na mashambulizi kama hayo ili kuwang’oa askari wa Kenya waliopo Somalia, ingawa maofisa wa polisi wana shaka na kuhusika kwa kundi hilo katika mashambulizi hayo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya ilithibitisha kuwa shambulio moja liliua watu 11 katika mji wa kibiashara wa Hindi, Kaunti ya Lamu, wilaya ile ile ambayo watu 65 waliuawa na watu wenye silaha mwezi uliopita.
Shambulio jingine lilitokea eneo la mbali kusini katika eneo la Gamba, ambako watu 18 waliuawa.
Katika eneo la Malamandi, Tarafa ya Hindi, Kaunti ya Lamu, polisi waliokota miili 11 ikiwa imeuawa kwa mapanga au risasi mashambani wakiwa ni wanaume.
Walioshuhudia walisema washambuliaji walikuwa vijana wa kiume waliovalia sare za msituni wakiwa wamebeba mapanga na bunduki huku wakizungumza zaidi lugha ya Kisomali.
Katika tukio la pili, watu waliojihami kwa silaha nzito walishambulia Kituo cha Polisi cha Gamba huko Garsen, Kaunti ya Delta Tana na kuua watu 18 akiwamo ofisa wa polisi aliyekuwa kazini na wafungwa.
Washambuliaji pia walimtorosha mtuhumiwa kinara wa shambulizi la hivi karibuni la Mpeketoni ambaye alikuwa akishikiliwa katika kituo hicho cha polisi.
Kundi la Al-Shabaab lilitoa taarifa likidai kuwa wapiganaji wake wameendesha shambulio jingine eneo hilo.
“Washambuliaji walirudi kambini kwao salama,” msemaji wa kijeshi wa Al-Shabaab, Abdulaziz Abu Musab, alisema jana.
Lakini, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipuuza madai ya Al-Shabaab mwezi uliopita na kuwalaumu wanasiasa kwamba ndiyo chanzo cha mauaji hayo.
Bila kujali nani anayelaumiwa kwa shambulio la safari hii, shambulio la juzi usiku litazidi kudhoofisha sekta ya utalii ambayo imeathirika vibaya na mashambulizi hayo.
Aidha, mashambulizi hayo yatazidisha hofu kuhusu udhaifu wa kiusalama nchini humo ikiwa ni siku moja kabla ya upinzani kuendesha mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika mjini Nairobi leo.
Akithibitisha tukio hilo, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Delta Tana, Mike Kimoko, alisema washambuliaji walimuua askari polisi aliyekuwa kazini na kuwatoa watu watano waliokuwa wakishikiliwa na kuwapiga risasi.
Aidha, waliwatoa raia watatu kutoka katika lori lililokuwa limewasili kituoni hapo na kuwaua kabla ya kutokomea kichakani.
Alisema kuwa washambuliaji walitumia fursa ya uwapo wa giza katika kituo cha polisi ambacho hakijaunganishwa na umeme na ilikuwa ngumu kueleza idadi ya washambuliaji.
Mashambulizi hayo yalikuja wakati Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto, akiwa eneo la pwani.
Ruto, alitarajia kutembelea Mpeketoni jana na kuhudhuria mkutano wa kidini wa kuomba amani.
Shambulio hilo limekuja wiki moja baada ya Kimoko kueleza wasiwasi wake kuhusu kuibuka kwa hali tete eneo hilo baada ya vipeperushi vya chuki kugundulika katika Kijiji cha Chakamba huko Kipini.
Vipeperushi hivyo vilionya baadhi ya jamii kuondoka eneo hilo kabla ya Julai 7, lakini Kimoko aliwatuliza wananchi kwa kuwataka wawe watulivu kwa vile maofisa wa usalama wanaendelea kuchunguza tukio.
Kwa mujibu wa Chifu Mkuu wa eneo hilo, Abdallah Shahasi, magaidi hao waliojihami kwa silaha kali zikiwamo bunduki na visu, walikuwa wakiwafyatulia risasi wakazi waliokuwa wakitembea njiani.
Shahasi alisema majangili hao pia walivamia ofisi yake na ile ya mkuu wa tarafa mjini Hindi ambapo waliiteketeza kwa moto.
Risasi zilizopigwa angani pia zilisikika mjini humo kwa zaidi ya saa moja.
Taharuki ilitanda usiku huo huku wenyeji wakilazimika kujifungia kwenye nyumba zao kwa kuhofia usalama.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Miiri Njenga, alithibitisha uvamizi huo huku akisema tayari ametuma maofisa wa polisi katika eneo hilo.
“Tumepeleka vikosi vya polisi wa utawala na GSU katika eneo hilo ili kudhibiti hali. Tunakabiliana na wavamizi na ningewasihi wakazi kuondoa hofu, watulie majumbani mwao na tutawajulisha habari kamili baadaye,” alisema Njenga.
Noordin Abdullahi ambaye ni mkazi wa Hindi mjini, alisema alisikia milio ya risasi takriban mita 300 kutoka nyumbani kwake mjini Hindi.
“Nimesikia milio kadhaa ya risasi, nilijifungia chumbani mwangu na kumpigia ofisa tawala wa wadi ambaye hakusita kupiga simu polisi. Kwa sasa kila mmoja yuko ndani ya nyumba kwa hofu,” anasema Abdullah kwa njia ya simu.