29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji Ubalozi wa Marekani Kenya

  • kenyaNAIROBI, KENYA

JARIBIO la kuushambulia ubalozi wa Marekani nchini Kenya, limesababisha Serikali ya Rais Barack Obama kuchukua hatua za kutangaza kuufunga kwa muda ubalozi wake nchini humo.

Hatua hiyo imetokana na tukio la kijana mmoja mwenye asili ya Kisomali kupigwa risasi juzi alasiri mbele ya ubalozi huo mjini Nairobi, baada ya kumchoma kisu Polisi wa Kenya ambaye alikuwa akisimamia ulinzi kwenye eneo la ubalozi huo.

Kutokana na tukio hilo, uchunguzi umeanzishwa mara moja licha ya kudaiwa kutokuwa na dalili zozote zinazoonyesha kama lilikuwa shambulizi la kigaidi.

Taarifa kutoka mjini humo zinaeleza kuwa polisi aliyekuwa amelengwa anatoka kikosi cha kijeshi cha polisi wa Kenya (GSU), ambacho pamoja na mambo mengine kinahusika kutoa ulinzi katika eneo lililo karibu na ubalozi wa Marekani nchini Kenya.

“Ni mpita njia ambaye alikuwa akitembea katika Mtaa wa Umoja wa Mataifa, alionekana kumwelekea kwa kasi askari huyo na kisha kumchoma kisu kichwani akiwa na lengo la kumnyang’anya silaha. Kufuatia kitendo cha kijana huyo ilimlazimu polisi huyo kujihami kwa kumpiga risasi na kufaulu kumuua papo hapo,” alisema Vitalis Otieno, mkuu wa polisi wa eneo la Gigiri.

Otieno alisema ofisa huyo aliyejeruhiwa alipelekwa mara moja hospitalini ambapo anaendelea vizuri.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mfanyakazi wa mgahawa uliopo karibu na eneo la tukio ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema aliona polisi akimpiga risasi mtu mmoja ambaye alikuwa na kisu mkononi baada ya kudondoka.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi nchini humo, kijana huyo ana umri wa miaka 24, ni mkazi wa Kaunti ya Wajir inayopakana na Somalia, lakini Jeshi hilo lilikataa kutoa maelezo zaidi kuhusu chanzo cha tukio hilo.

Tukio hilo limeonekana kuzua hali ya taharuki kiasi cha kuwalazimu askari wa shirika la kijasusi la FBI kuingilia kati na kuimarisha ulinzi katika eneo hilo la ubalozi.

Aidha, tukio hilo ni miongoni mwa mengi yaliyowahi kutokea nchini Kenya na inadaiwa kuwa ipo hofu dhidi ya vitendo visivyo vya kawaida na ambavyo vinadhaniwa kuwa vya kigaidi.

Kulingana na taraifa ya Kamanda Otieno, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini dhamira ya kijana huyo na kilichopo nyuma ya pazia, licha ya kudhaniwa kuwa ni mpiganaji wa kundi la kigaidi la Al Shabab.

UGAIDI WA GARISSA

Matukio ya kigaidi nchini humo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hali ambayo imewahi kulitikisa taifa hilo pamoja na kudhoofisha uchumi kufuatia sekta ya utalii kukosa pato la nje. Matukio hayo yamesababisha hofu ya usalama wa wananchi na wageni.

Tukio la kigaidi lililowahi kutokea Kenya ni lile la Alhamisi ya Aprili 2, mwaka jana ambapo wanafunzi 147 waliuawa kufuatia shambulizi la kigaidi lililofanyika huko Chuo Kikuu cha Garissa, Mashariki mwa Kenya.

Tukio hilo lilishuhudia zaidi ya watu 75 wakijeruhiwa wakiwemo maofisa wa Jeshi la Polisi nchini humo.

Shambulizi la Chuo Kikuu cha Garissa lilitokana na watu wenye silaha kuvamia chuoni hapo na kuanza kufyatua risasi ovyo na kuwashikilia mateka wanafunzi kadhaa.

Washukiwa wakubwa wa tukio la Garissa walikuwa ni kundi la kigaidi la Al-Shabab ambalo lilitoa taarifa na kudai kuhusika na shambulizi hilo.

SHAMBULIO LA MADUKA YA WESTGATE

Septemba 21, 2013 ni siku ambayo iliacha kumbukumbu ya kutisha kwa wananchi wa Kenya. Ni siku ambayo kikundi cha kigaidi cha Al Shabab kilitekeleza mauaji ya kutisha kwenye majengo ya biashara ya Westgate (Westgate Shopping Mall) jijini Nairobi na kuacha maelfu ya vifo na majeruhi.

Takwimu za karibuni kabisa za Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, zinaonesha kuwa shambulio hilo la kigaidi lilisababisha watu 67 kuuawa huku hatima ya watu 39 ikiwa haijulikani hadi sasa.

Wakati Wakenya na walimwengu wakiwa wanajiuliza maswali mengi yasiyo na majibu kuhusiana na shambulio la kundi la Al Shabab jijini Nairobi, wanachama wa kundi hilo walifanya shambulio jingine katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab katika mpaka wa Kenya na Somalia.

UGAIDI HOTELINI

Mwaka 2012 kulitokea tukio la kigaidi katika Hoteli ya Bella Vista maarufu sana kwa watalii na wenyeji iliyopo mjini Mombasa ambapo ilishambuliwa kwa maguruneti na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Taarifa ya Mkuu wa Jeshi la Polisi mjini humo, Ambrose Munyasya, wakati huo ilisema watu watano walijeruhiwa vibaya katika tukio hilo na kwamba magaidi wa Al Shabab walihusika kwenye shambulio hilo ambalo lilisababisha uharibifu wa magari sita yaliyokuwa yameegeshwa kando ya hoteli hiyo.

Inadaiwa kuwa watu wawili walikwenda hotelini hapo wakitaka kuruhusiwa kuingia. Lakini walipotakiwa kupekuliwa na maaskari wa hoteli hiyo walikataa na ndipo wakarusha maguruneti hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles