29.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji Simiyu yang’oa kamanda wa polisi


DERICK MILTONBUSEGA

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amemuondoa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Deusdedit Nsimeki kwa kushindwa kudhibiti matukio ya uhalifu likiwamo wimbi la mauaji ya watoto,  mkoani humo hivi karibuni.

Uamuzi huo aliutangaza juzi jioni alipozungumza na wananchi mjini Lamadi Wilaya ya Busega.

Alisema amechukua uamuzi huo baada ya kamanda huyo kulalamikiwa na wananchi kushindwa kudhibiti hali hiyo.

Alisema pamoja na hali hiyo ni lazima kila aliyepewa jukumu ndani ya Jeshi la Polisi atimize wajibu wake ikiwamo kulinda raia na mali zao.

“Kutokana na matukio hayo tayari nimemwondoa aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa, Deusdedit Nsimeki na kumleta mwingine (hakumtaja jina),” alisema IGP Sirro.

Alisema  mbali na wananchi kumlalamikia kamanda huyo wa polisi,   bado alionekana kushindwa kukomesha matukio hayo, kazi ambayo alitakiwa kuifanya.

“Mbali na nyie kumlalamikia RPC hata alipokuja kwangu nilimuuliza swali moja, wewe nilikuteua kwenda huko kunisaidia kukomesha uhalifu, sasa kwa nini bado matukio yanaendelea? Na mimi nikaona kazi imemshinda,” alisema.

Pamoja na kuchukua uamuzi huo aliwataka wananchi kutowalalamikia askari  wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao  badala yake wawataje baadhi ya askari wahusika na si jeshi lote.

Hadi sasa imeripotiwa   watoto watatu   na wanawake wawili wameuawa na kunyofolewa baadhi ya viungo vyao tangu Oktoba 10 mwaka jana hadi mwaka huu.

Matukio hayo yanahusishwa na imani za ushirikina na mpaka sasa   watu 12 wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kuhusika katika matukio hayo.

Kabla ya kuzungumza na wananchi hao alifanya kikao cha ndani cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kilichodumu  kwa saa mbili.

Sirro alisema   tayari ameongeza nguvu kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi  kuweza kushughulikia   matukio ya mauaji Lamadi.

Aliahidi kukomesha   mtandao mzima wa wahalifu.

“Kuna watu bado wanaamini kupata samaki wengi mpaka watumie njia za ushirikina, mimi bado naikumbuka Lamadi hii tabia ilikiwapo zamani na wahusika wakuu walikuwa wazazi wa watoto.

“Sasa nimeagiza, watafutwe hata hao ambao walihusika katika matukio kama haya huko zamani, tuone kesi zao zilienda vipi na tujue wapi tunaanzia, lakini elimu inahitajika zaidi kwa wananchi,” alisema IGP Sirro.

Alisema ndani ya siku 10 atahakikisha wahusika wote wanapatikana na kuchukuliwa hatua za sheria.

MAUAJI NJOMBE

Sirro, vilevile alisema tayari jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limefanikiwa kudhibiti matukio ya mauaji dhidi ya watoto mkoani Njombe.

Alisema wahusika wa matukio hayo wote wamekamatwa wakiwamo vijana wawili ambao wamekiri kuhusika na kuwaua baadhi ya watoto kutokana na ugomvi wa familia zao pamoja na kutumia madawa ya kulevya.

“Kijana mmoja alikuwa na ugomvi wa  familia akakiri kuhusika   kuua watoto   kulipiza kisasi, mwingine alikuwa mvuta bangi na madawa ya kulevya, wote tumewakamata na watafikishwa mahakamani muda wowote,” alisema Sirro.

Alisema jeshi hilo halitakubali mtu yeyote awavuruge wananchi, kuhatarisha amani ya nchi na kuvuruga amani iliyopo kwa sababu  wahusika wote watachukuliwa hatua kali za  sheria.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, alimweleza IGP Sirro kuwa kuhusiana na matukio hayo wamechukua hatua za awali ikiwamo wananchi kupiga kura za siri huku baadhi ya watuhumiwa kukifikishwa mahakamani.

Alisema suala la kupiga kura za siri lilitokana na uamuzi wa wananchi ambao walipona ni vema kutumia njia hiyo ambayo waliiamini na kuweza kuwataja baadhi ya wahusika wa matukio hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles