23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ngono kwa mdomo inavyosababisha saratani

*Vijana wa miaka 20 hadi 40, waathirika wakubwa

*Utafiti wa Ocean Road 2008, alisema 90 kansa ya koo wanaume, asilimia 10 wanawake.

*Ocean Road kuna ongezeko la wagonjwa wa saratani ya koo 511 ndani ya kipindi cha miaka 12.

*Mama mwenye virusi vinavyosababisha saratani hiyo akijifungua anaweza kumuweka mtoto kwenye hatari

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

IKIWA wewe ni miongoni mwa watu wanaopenda kushiriki mapenzi kwa njia ya mdomo (kunyonya sehemu za siri za mwezi wako), unapaswa kutambua kwamba unajiweka kwenye hatari ya kuishia kupata saratani ya koo.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu hivi karibuni, Daktari Bingwa wa Idara ya Upasuaji wa Magonjwa ya Masikio, Pua, Koo na Vivimbe vya Kichwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Tawi la Mloganzila (MAMC), Godwin Mfuko, alifafanua kwa kina juu ya suala hilo.

Alisema watu wanaojihusisha na ngono kwa njia hiyo wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa uitwao kitaalamu Recurrent Laryngeal papillomatosis (RLP).

“Hii ni aina nyingine ya ugonjwa ambao unafanana na saratani, lakini si saratani moja kwa moja, unaweza kugeuka kuwa saratani ikiwa mtu hatapata matibabu yanayostahili kwa wakati.

“Yaani unakuta kuna vivimbe vingi vimeota kooni, lakini vyenyewe si saratani, vivimbe hivyo hukaa kama mfano wa vioto (majani) pale kooni na hivyo kumfanya mhusika ashindwe kupumua vizuri.

“Ikiwa mgonjwa hatapatiwa matibabu mapema, ile ‘infection’ (maambukizi) inaweza kupenya kwenye chembe chembe hai za mwili na hivyo kugeuka kuwa saratani, tunapokea watu wengi wanaougua ugonjwa huu hivi sasa,” alifafanua.

Watoto nao waugua

Bingwa huyo wa Mloganzila alisema katika kliniki zao wanapokea zaidi watoto kati ya miaka miwili hadi minne na vijana kuanzia umri wa miaka 20 hadi 40, wanaokabiliwa na ugonjwa huo.

“Watoto hupata maambukizi kutoka kwa mama zao wakati wa kuzaliwa kwa njia ya kawaida, ikiwa mama ana maambukizi ya kirusi cha Human Papilloma (HPV) ukeni, huweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa kujifungua,” alibainisha.

Alisema kwa upande wa vijana wa miaka 20 hadi 40, katika kipindi hicho wanakuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi hayo kwani ndicho kipindi ambacho wengi huanza kushiriki ngono.

 “Ugonjwa huu hutokana na maambukizi ya kirusi hicho cha HPV ambacho hukaa sehemu za siri na ndicho ambacho husababisha saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake,” alibainisha.

Wengi hutibiwa kama pumu

Dk. Mfuko alisema watoto wengi wanaowapokea katika kliniki yao huwa wamepitia na kutibiwa kwenye hospitali mbalimbali kama wagonjwa wa pumu.

“Nimeeleza awali kwamba, mtoto anakuwa kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu kama mama ana maambukizi ya HPV ukeni, anapozaliwa kwa njia ya kawaida.

“Watoto wengi wanaokabiliwa na ugonjwa huu, dalili ya kwanza ambayo huonesha ni pale wanapofikisha umri wa miaka miwili, hushindwa kupumua vizuri, ndiyo maana utaona wengi hutibiwa kama pumu, lakini tunapowachunguza tunakuta wana vinyama vimeota kama majani kooni.

“Majibu ya vipimo hutueleza wanaugua RLP, kwa kawaida vinyama hivyo vinavyokuwa vimeota, vinapokatwa huwa na tabia ya kuota tena, mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji hata mara 30, unakuta vinajirudia kuota,” alisema.

Alisisitiza kuwa kimsingi jamii inapaswa kuelewa kwamba, ngono kwa njia ya mdomo pekee (kunyonya sehemu za siri) hakusababishi mtu kupata saratani hiyo moja kwa moja.

“Isipokuwa kuna huo uhusiano wa karibu na mtu anakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ikiwa huyo anayeshiriki naye ana maambukizi ya kirusi hicho cha HPV,” alisema.

Alisema wapenzi wanaponyonyana sehemu za siri ikiwa mmoja ana maambukizi ya kirusi hicho, huingia kinywani na kwenda moja kwa moja katika chembe chembe hai za mwili.

“Kwa hiyo ukiniuliza iwapo ngono kwa njia ya mdomo inasababisha saratani, nitakwambia hakuna jibu la moja kwa moja, kwa sababu mtu anaweza kupata maambukizi ya kirusi hiki lakini asipate saratani.

“Atapata saratani ikiwa kirusi cha HPV kitaenda kuathiri chembechembe hai za mwili na kuingiza vinasaba vyake na hivyo kuzigeuza tabia yake na kuzifanya zikue bila mpangilio,” alifafanua.

Kinachotokea

“Hivyo, mtu akifanya ngono kwa njia hii hujiweka kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya koo, kama yule anayemlamba anakuwa na maambukizi ya kirusi hiki.

“Kwa sababu akipata maambukizi ya kirusi hicho cha HPV kikiingia mwilini mwake, kinaweza kwenda kuathiri chembechembe hai za mwili zilizopo kooni.

“Kirusi cha HPV kikiingia kooni kinaweza kuathiri chembechembe hai za mwili na kusababisha ‘infection’, kirusi hiki kinapoingia kwenye seli huingiza vinasaba vyake, ile seli ya mwili inageuka, inakuwa na kinasaba cha kirusi hiki.

“Hapo kirusi kinakuwa na uwezo wa kuanza kubadilisha ile seli na hivyo kuwa saratani, tunajua tabia ya saratani inapoingia mwilini huwa inabadilisha tabia ya seli.

“Kitaalamu tunajua wazi seli za mwili huwa zinakua na kugawanyika taratibu, lakini saratani inapoingia mwilini seli za mwili huathirika na kuanza kukua kwa haraka na kugawanyika bila mpangilio.

“Kwa sababu kile kirusi kinabadilisha kabisa ukuaji wa seli ndiyo maana unakuta mtu ameota nyama kubwa shingoni, yale ni matokeo ya kukua bila kudhibitiwa kwa zile seli za mwili,” alisema.

Aliongeza: “Hata hivyo, uvimbe wa saratani unapoota mara nyingi huwa unaweza usiwe na maumivu ya aina yoyote ile, lakini unakua unaongezeka kwa kasi kuliko kawaida.

Kijana anena

Mariam Isaya (si jina lake halisi), Mkazi wa Bunju, alisema hupendelea zaidi kushiriki ngono na mpenzi wake kwa njia ya mdomo.

“Huwa napata hisia zaidi nikifanya hivyo, napenda mpenzi wangu anavyonieleza jinsi anavyojisikia pindi ninapomfanyia kitendo hicho,” alisema.

Alisema mpenzi wake pia huwa anashiriki naye ngono kwa njia ya mdomo na kwamba, kila wanapokutana lazima wafanye kitendo hicho.

“Sina hakika na wala sijui kwamba kitendo hicho kinaweza kutusababishia kupata saratani, tumeanza kufanya hivyo kwa muda mrefu sasa na wala sifikirii na sidhani kama mpenzi wangu anafikiria kuacha, kuna raha ya kipekee,” alisema.

Imegawanyika

Dk. Mfuko alisema saratani ya koo imegawanyika katika sehemu mbili, ipo inayotokea katika koo la chakula na nyingine katika koo la hewa.

Alisema koo la chakula lipo katika sehemu ya juu na mwendelezo wake huishia kwenye tumbo la chakula na kwa upande wa koo la hewa lenyewe huunganika hadi kwenye mapafu.

“Mtu akifanya ngono kwa njia ya mdomo anaweza pia kupata saratani kwenye kinywa, sehemu ya nyuma ya ulimi, sehemu ya juu au eneo lolote hadi kwenye koo,” alibainisha.

Aliongeza: “Hizi saratani za koo la chakula nazo zimegawanyika katika sehemu kuu tatu, ipo ambayo inahusisha zile zinazogusa misuli ambako ‘vocal cord’ (sauti) ndiko huwa zinatoka.

“Ipo ambayo hutokea katika eneo la chini ya zile ‘vocal cord’ na nyingine hutokea eneo la juu, zote zinaweza kuwa na dalili zinazoshabihiana,” alibainisha.

Utafiti wa Ocean Road

Daktari huyo alisema mwaka 2008 hadi 2011 Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), ilifanya utafiti uliohusisha wagonjwa kati ya 87 hadi 90 wa saratani ya koo ambao walilazwa kwa matibabu katika kipindi hicho.

Alisema matokeo ya utafiti huo yanaeleza karibu asilimia 90 ya wagonjwa waliokuwa wamepata saratani hiyo, walikuwa wanaume, wanawake walikuwa asilimia 10 tu.

“ORCI walifanya utafiti huo kuangalia matokeo ya tiba, aina ya saratani na sehemu gani ya koo ilikuwa imeathirika kwa wagonjwa hao, waliangalia visababishi vitatu, walihoji iwapo walikuwa ni wavutaji sigara, watumiaji wa pombe au vyote viwili kwa pamoja.

“Matokeo yao yanaonesha karibu asilimia 70 walionekana walikuwa wanatumia pombe na sigara, asilimia 12.5 walikuwa watumiaji wa sigara pekee na asilimia 18 walikuwa watumiaji wa pombe, katika utafiti huo hawakuhoji kabisa kuhusu ngono kwa njia ya mdomo,” alisema.

Tafiti ya Marekani

Dk. Mfuko alisema, nchini Marekani waliwahi kufanya utafiti na kugundua kwamba asilimia 35 ya wagonjwa wenye saratani ya koo nchini humo, wana ‘infection’ ya kirusi hiki cha HPV.

“Kule ngono kwa njia hii ni jambo la kawaida, maana yake ni kwamba kati ya watu 100 wenye saratani ya koo watu 35 wana maambukizi ya kirusi hiki cha HPV,” alifafanua.

Aliongeza: “Inaonesha kwamba ingawa inawezekana si kirusi hiki kiliwasababishia moja kwa moja kupata saratani, lakini kwa utafiti wa Marekani inaonesha watu wanaokunywa pombe wapo kwenye hatari zaidi ya kupata saratani hiyo kuliko wasiotumia.

Dalili

Bingwa huyo wa Mloganzila alisema, miongoni mwa dalili za awali kwamba mtu anakabiliwa na saratani hiyo, ni kupata sauti inayokwaruza, maumivu wakati wa kumeza chakula, shida ya kupumua au maumivu ya koo.

“Mtu akipata shida ya kupumua anakuwa anapata shida akivuta hewa ndani huwa inatoa sauti fulani kwa sababu ile sehemu inakuwa imeziba,” alisema.

Aliongeza: “Ikiwa saratani ipo kwenye koo la hewa mgonjwa hupumua kwa shida, sauti haitoki vizuri au sauti inakuwa inatokea kwa ndani pindi anapovuta hewa (stridor).

“Ili kumsaidia mgonjwa wa aina hii huwa inabidi tumfanyie upasuaji wa kutengeneza njia mbadala ya kupitishia hewa, kwani tukimwacha anaweza kukosa hewa na kupoteza maisha,” alisema.

Alifafanua, ikiwa ni saratani imeshambulia katika koo la chakula mgonjwa hushindwa kumeza chakula vizuri au hupata maumivu makali wakati wa kumeza.

Hatari zaidi

Alisema saratani inayohusisha koo la chakula ni hatari zaidi kwani sehemu hiyo ni pana, hivyo dalili huchelewa kujionesha na huanza kujitokeza wakati tayari ikiwa imeshasambaa sehemu kubwa kuliko saratani ya koo la hewa.

“Mara nyingi saratani ya koo la hewa hugundulika mapema kwa sababu inapoanza tu mara nyingi sauti huwa inashindwa kupita, hivyo mtu anapokuja hospitalini anagundulika mapema na kupatiwa matibabu mapema, anapona.

“Lakini kwa upande wa koo la chakula  kwa sababu dalili huchelewa kujitokeza, wengi huja hospitalini wakati tayari inakuwa imeshaanza kusambaa na ikiwa katika hatua za juu (tatu na nne) ambazo kwa kawaida huwa ngumu kutibika,” alisema.

Aliongeza: “Saratani ya koo la chakula ikisambaa mno huweza pia kuathiri koo la hewa, wakati mwingine pia huweza kusababisha tezi zilizopo kooni nazo kuvimba.

Uchunguzi

Bingwa huyo alisema huwa wanalazimika kuchukua sampuli ya kinyama kutoka kwa mgonjwa na kwenda kukichunguza maabara ambako huwa na uwezo wa kujua ni aina gani ya saratani (koo la chakula au la hewa) na imefikia hatua gani.

“Tunashirikiana kwa ukaribu na wataalamu wenzetu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI),” alibainisha.

Wanaume

“Kundi la wanaume ndilo lililopo kwenye hatari zaidi kupata saratani hii ikilinganishwa na wanawake kwa sababu kuu mbili, kundi hili ndilo linawatumiaji wengi wa pombe na sigara.

“Hata idadi ya wanaokuja kliniki kwa matibabu tunaona wengi ni wanaume watu wazima kuanzia umri wa miaka 50 na kuendelea,” alibainisha.

Alisema japo katika utafiti ule wa ORCI hawakuhusisha ngono kwa njia ya mdomo, waliangazia zaidi matumizi ya pombe na sigara, hivi sasa kuna utafiti ambao tunafanya.

“Tunapochukua historia zao huwa tunawauliza iwapo wamewahi kushiriki ngono kwa njia ya mdomo, bado utafiti huo unaendelea utakapokamilika tutatoa matokeo yake,” alibainisha.

Itaendelea Kesho..

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles