Dixon Busagaga-Moshi
MAHAKAM Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, imetupilia mbali hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi wakipinga kupokelewa kwa maelezo ya ungamo ya Hamis Chacha, mshtakiwa wa kwanza katika shauri la mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi Humphrey Makundi.
Mbali na kutupilia mbali hoja za upande wa utetezi, Mahakama pia imepokea maelezo ya kukiri kutenda kosa kwa mshtakiwa wa kwanza Hamis Chacha, aliyoyatoa kwa mlinzi wa amani yatumike kama kielelezo katika ushahidi wa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Moshi Mjini, Irene Mushi.
Mahakama imetoa uamuzi huo mdogo katika kesi hiyo ndani ya shauri la msingi la mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi Humphrey Makundi, baada ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Firmin Matogoro kupitia kwa kina hoja za pande zote .
Akisoma maelezo ya hukumu Jaji Matogoro, alisema Wakili Gwakisa Sambo wa upande wa utetezi aliwasilisha hoja kupinga kupokelewa kwa kielelezo hicho kwa kueleza pungufu mkubwa wa kisheria na kwamba haikukidhi masharti ya uwiano.
Alisema hoja za upande wa utetezi zilikuwa katika maeneo mawili huku ya kwanza wakieleza kuwa utaratibu wa uchukuaji wa maelezo ya mshtakiwa wa kwanza, Hamis Chacha, haukufuata sheria na hakuweza kueleza muda wa wapi mshtakiwa alilala kabla ya kufikishwa mbele ya mlinzi wa amani.
Jaji Matogoro, alisema hoja nyingine ya upande wa utetezi waliielekeza kwenye eneo uhiari endapo mshtakiwa Hamis Chacha, alitoa maelezo ya ungamo mbele ya mlinzi wa amani bila ya kushurutishwa, kupigwa, kulazimishwa ama kuahidiwa .
Alisema upande wa utetezi ulienda mbali zaidi ukieleza kuwa maelezo hayo yalichukuliwa nje ya muda unaotakiwa kisheria, akinukuu vifungu vya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, kifungu cha 50 na 51 kinachoelekeza juu ya uchukuaji maelezo .
Baada ya kusoma hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi, Jaji Matogoro akasoma hoja zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri wakipinga hoja za upande wa utetezi ikiwemo kifungu cha 50 na 51 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ukieleza kuwa vifungu hivyo vipo kwa ajili ya maofisa wa Polisi na si mahakimu.
Akitoa uamuzi wa Mahakama Jaji Matogoro, alisema kulingana na maelezo hayo yameonesha muda yalipochukuliwa tofauti na hoja kwamba maelezo yalitolewa nje ya muda kama walivyoeleza saa zisizidi saa 8 na kwamba hakuna muda wa ukomo wa kuandika maelezo ya ungamo.
Alisema tarehe imeonyesha alikamatwa Novemba 17, 2017 katika Shule ya Sekondari ya Scholastica iliyopo Himo na baadae alipelekwa Kituo cha Polisi Himo kabla ya kupelekwa Kituo cha Polisi Moshi Mjini majira ya saa moja jioni na kutupilia mbali hoja hiyo na kwamba fomu ya mlinzi wa amani haina sehemu iliyomtaka kujaza Mshtakiwa alilala wapi kabla ya kufikishwa kwake.
Jaji Matogoro, alisema Mahakama imemuona shahidi wa kwanza katika kesi ndani ya kesi ya msingi, Hamisi Chacha ambaye pia ni mshtakiwa wa kwanza katika shauri hilo kuwa ni muongo kulingana na maelezo aliyotoa wakati wa kutoa ushahidi.
“Maelezo aliyatoa Chacha ni yale aliyoieleza mahakama juu ya kukamatwa kwake, kupigwa, kuteswa kwa kuchomwa pasi ya umeme, kupigwa shoti ya umeme, kuwekewa chupa ya bia sehemu yake ya haja kubwa pamoja na kulazwa kwenye chumba chenye maji kwa kile alichoeleza kushinikizwa kueleza yale yaliyotakiwa na askari Polisi.
“Kama Mshtakiwa aliteswa kama alivyoeleza basi mawakili wa upande wa utetezi walikuwa na nafasi ya kuwauliza maswali , shahidi wa tatu na nne , ambao ni Inspekta Fredy na Inspekta Tenga waliotajwa na mshtakiwa katika maelezo yake kuwa ndio walihusika katika kumtesa .
“Mshtakiwa wa kwanza amejikanganya katika majibu yake, mshtakiwa amedanganya alipoulizwa na upande wa Jamhuri, Mahakama imemuona si shahidi wa kweli na amesema uongo, hakuna sababu za msingi na kurudisha pingamizi la utetezi natupilia mbali ombi hilo,” alisema Jaji Matogoro wakati akitoa uamuzi huo wa Mahakama.
Shauri hilo linalovuta hisia za wananchi wengi linaendelea katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, mbele ya JajiFirmini Matogoro kwa hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa Jamhuri.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri unaaongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Joseph Pande akisaidiana na mawakili wenzake wa serikali ambao ni Abdalah Chavula, Omari Kibwana na Lucy Kiusa .
Upande wa utetezi unaongozwa na mawakili wa kujitegemea Elikunda Kipoko na Gwakisa Sambo ambao wanamtetea mshtakiwa wa pili, Edward Shayo huku Wakili David Shilatu anamteta mshitakiwa wa kwanza, Hamis Chacha na Wakili Patrick Paul naye anamtetea mshtakiwa wa tatu Mwalimu Laban Nabiswa.
Mwanafunzi Humphrey Makundi aliyekuwa akijiandaa na mitihani ya Taifa ya Kidato cha Pili alitoweka shuleni hapo mnamo Novemba 6, 2017 na baadaye ilibainika ameuawa na watu wasiojulikana baada ya mwili wake kufukuliwa katika Makaburi ya Karanga mjini Moshi.
Hali hiyo ilikuja baada ya kuwepo kwa taarifa za mtu aliyezikwa katika makaburi hayo ambaye mwili wake uliokotwa Mto Ghona, mita 300 jirani na shule hiyo.