23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

‘Kukaa muda mrefu safarini chanzo cha kiharusi’

TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

WATU wanaosafiri umbali mrefu wakiwa wamekaa wako hatarini kupata kiharusi kinachotokana na kuziba  mishipa ya damu ya kichwani. Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam juzi, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Damu wa Hospitali ya Aga Khan, Dk. Mugisha Clement alisema hatari hiyo inatokana na damu kuganda miguuni.

“Damu inazunguka ikitokea miguuni, ikiwa msafiri amekaa muda mrefu bila kutembea husababisha kuwapo  vidonge vya damu ambavyo kama mwili ukishindwa kuviyeyusha hufika kichwani na kuziba mishipa ya damu ya ubongo,” alisema Dk. Mugisha.

Alisema kutembea kunasaidia kusukuma damu kutoka miguuni kwenda kwenye moyo hadi kichwani hivyo kukaa muda mrefu kunapunguza kasi ya damu kusukumwa  kuanzia miguuni.

Dk. Mugisha alisema ugonjwa huo pia unachangiwa na matumizi ya mafuta yenye lehemu (cholesterol) ambayo hujenga ukuta katika mishipa ya damu na hutoa vibonge ambavyo huingia kwenye mzunguko wa damu hadi kichwani na kuziba mishipa ya damu.

“Ugonjwa huo pia huchangiwa iwapo mtu ana matatizo ya kukakamaa kwa mishipa ya damu kunakotokana na kuugua ‘tonses’ pamoja na kubadilikabadilika kwa mapigo  ya moyo, ambavyo vyote husababisha kuwapo vidonge vya damu katika mzunguko,”alisema Dk Mugisha.

Daktari huyo bingwa alisema ingawa awali ugonjwa huo uliwaathiri zaidi watu wenye umri wa kuanzia miaka 55 lakini kutokana na mifumo ya maisha ya sasa umri wowote unaweza kumpata.

Dk. Mugisha alitoa wito kwa ndugu na jamaa wa mgonjwa kuhakikisha wanamfikisha mgonjwa hospitali ndani ya saa moja hadi tatu baada ya kupatwa na kiharusi kupatiwa matibabu ya haraka kabla hajaathirika zaidi. “Ugonjwa huu unatibika hospitalini iwapo mgonjwa atawahishwa mapema na kupatiwa matibabu ndani ya saa sita hadi nane ingawa inategemea alivyoathirika,” alisema Dk. Mugisha.

Aliwashauri watanzania kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya vyakula vyenye mafuta yenye lehemu  kuepuka tatizo hilo. Akizungumzia dalili za ugonjwa huo, Dk.Mugisha alisema mgonjwa hupoteza nguvu upande mmoja wa mwili ukiwamo mguu, mkono, mdomo na jicho.

Alisema tofauti ya ugonjwa wa kiharusi kinachotokana na kuziba   mishipa ya damu na kile cha kupasuka   mishipa ya damu kichwani ni kwamba “Ugonjwa huu mgonjwa hataumwa kichwa,” alisema na kuongeza: “Pia kuna tofauti kati ya ugonjwa huu na maambukizi ya virusi vya mafua ambayo nayo husababisha upande mmoja wa uso kukosa nguvu ambako katika mafua mgonjwa huumwa kichwa hasa usawa wa macho”.

Dk. Mugisha alisema matibabu ya ugonjwa huo yanahusisha kundi la wataalamu wakiwamo madaktari wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, wanasaikolojia, wataalamu wa chakula  na lishe, wataalamu wa mazoezi, madaktari wa kawaida pamoja na ndugu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles