22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Matumizi ya dola yashika kasi Dar

dola* Masaki, Mikocheni, Upanga na Mbweni zaongoza

BAKARI KIMWANGA, DODOMA NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

MATUMIZI ya dola ya Marekani dhidi ya shilingi ya Tanzania yameshika kasi Dar es Salaam.

Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao umebaini matumizi ya dola katika Jiji la Dar es Salaam yamefikia asilimia 0.3, ikiwa ni tofauti na mikoa mingine.

Utafiti huo umefanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Mwanza na mikoa mitatu ya visiwani Zanzibar.

Katika utafiti huo, imebainika kuwa mfanyabiashara au mtoa huduma katika maeneo hayo hakuwa tayari kukubali malipo kwa fedha za Kitanzania, huku akitaka malipo ya dola ya Marekani kutokana na wateja wao kuwa wageni wa kitalii.

Umebainisha utafiti huo kuwa malipo hayo yalifanyika kwa ajili ya ofisi za kukodisha na nyumba za kupanga katika baadhi ya maeneo hasa ya Masaki, Mikocheni, Upanga na Mbweni, Dar es Salaam. Na kwa Mkoa wa Arusha eneo la Kilombero na barabara zinazokwenda maeneo ya watalii pia wanatumia dola.

 

UNUNUZI WA BIDHAA

Kwa mujibu wa utafiti huo, inaelezwa kwa kawaida wakati wa ununuzi wa bidhaa na huduma, Watanzania hawana utamaduni wa kubeba fedha za kigeni katika pochi zao na kama ingekuwa hivyo wangeweza kushindwa kufanya shughuli kwa kutumia fedha za ndani.

Hali hiyo inatoa baadhi ya ushahidi kwamba kiwango ambacho fedha za kigeni hutumika kwa shughuli za ndani si muhimu. Katika jitihada za kutoa ushahidi wa kuaminika juu ya hilo, watafiti walitaka kutambua fedha ambazo wafanyabiashara nchini Tanzania wangependelea kupokea kama malipo ya huduma na bidhaa wanazouza.

“Kama jambo hili lilikuwa linafanywa kwa siri katika maduka makubwa (shoppers). Matokeo yanaonyesha matumizi ya dola kwa ajili ya shughuli za ndani si muhimu. Asilimia 0.1 tu ya washiriki walitaka malipo kwa dola, huku kwa upande wa Zanzibar, walikuwa tayari kukubali malipo ya fedha za Kitanzania, hata kama bei waliitaja kwa kiwango cha dola.

“Asilimia 3.1 ya washiriki kwa upande wa Bara na asilimia 4.5 Zanzibar, walikuwa tayari kukubali malipo ya dola au shilingi za Kitanzania, wakati asilimia 96.8 ya washiriki (Bara) na asilimia 95.5 (Zanzibar) hupendelea malipo kwa shilingi ya Tanzania,” ilieleza sehemu ya taarifa ya utafiti huo.

 

MBINU

Mbinu zilizotumika katika utafiti huo, ni pamoja na sampuli ya juu ambapo watu 3,945 walihojiwa kwa upande wa Tanzania Bara na 290 kutoka Zanzibar.

Kwa upande wa Bara, sampuli ilichukuliwa mikoa sita ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Mwanza, wakati Zanzibar sampuli ilichukuliwa kutoka mikoa mitatu ya Mjini Magharibi, Pemba Kaskazini na Kusini Pemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles