Na GUSTAPHU HAULE-PWANI
JESHI la Polisi, Mkoa wa Pwani, limesema matukio ya uhalifu wa kutumia silaha, mauaji, ubakaji na uvunjaji, yamepungua katika kipindi cha mwaka 2017.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na matukio ya uhalifu yaliyotokea katika kipindi cha mwaka 2017.
Kamanda Shanna, alisema kwamba, mwaka 2016 matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha yalikuwa 31 wakati mwaka 2017 matukio hayo yalipungua na kufikia manane.
Kwa upande wa matukio ya ubakaji, alisema mwaka 2016 yalikuwa 191, lakini mwaka 2017 yalipungua na kufikia 21 na makosa ya mauaji yamepungua kutoka 126 hadi matukio 34.
“Makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu mwaka 2016 yalikuwa 112 na mwaka 2017 yalipungua mpaka kufikia 43 na matukio ya uvunjaji yalipungua kutoka 771 hadi 233.
“Kupungua kwa matukio hayo katika kipindi cha mwaka 2017, kumetokana na jitihada za Jeshi la Polisi zinazofanywa kupitia operesheni mbalimbali zikiwamo kuweka doria za mara kwa mara.
“Pia, wananchi nao kwa upande wao wamekuwa na mchango mkubwa kwetu kwa sababu mara kadhaa wamekuwa wakitoa ushirikiano na kutufanya tufanye kazi zetu kwa mafanikio zaidi,” alisema Kamanda Shanna.
Akizungumzia mwaka 2018, kamanda huyo alisema wamejipanga kuimarisha doria na operesheni mbalimbali ili kuhakikisha matukio hayo ya uhalifu yanazidi kupungua.