27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MATOKEO YA TAFITI HIZI YANAWEZA KUKUHAMASISHA KUANZA MAZOEZI


Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.

WAKATI mwingine tunakata tama kufanya mambo Fulani kwa kukosa sababu zinazotuhamasisha kufanya mambo hayo. Na mara nyingi tunakosa sababu kutokana na kutokuwapo kwa shaidi za kitaalamu zinazotuhamasisha kufanya hivyo. Leo tutachambua matokeo ya tafiti kubwa kabisa duniani kuhusu umuhimu wa mazoezi katika maisha na kwa afya zetu.

Watu wanaofanya mazoezi mara kwa mara wanauwezekano mdogo  wa kupoteza maisha kunakosababishwa na matatizo mbalimbali

Katika utafiti uliohusisha wanaume na wanawake wa umri wa kati, ambapo watu hawa walifuatiliwa kwa muda wa takribani miaka nane, ilionekana kwamba, ukilinganisha na wale wasiofanya mazoezi, wengi wa wanawake na wanaume waliokuwa wakifanya mazoezi mara kwa mara hawakupoteza maisha yao katika kipindi hicho cha miaka nane. Hii inamaana kwamba kundi kubwa la waliopoteza maisha lilitoka katika kundi la watu wasiofanya mazoezi. Tafiti za hivi karibuni zimedhihirisha umuhimu huu wa mazoezi kwa kuonyesha kwamba, watu wasiofanya mazoezi mara kwa mara wanaouwezo wa kupoteza maisha mara mbili zaidi ya wale wanaofanya mazoezi mara kwa mara. 

Kupunguza makali na kuzuia vifo kwa watu wenye magonjwa ya moyo

Mnyumbulisho wa muunganisho wa matokeo ya tafiti zaidi ya 48 (meta-analysis) zilizofanyika katika sehemu mbalimbali duniani zinaonyesha kwamba, kufanya mazoezi mara kwa mara huweza kupunguza makali na hata kuponya baadhi ya maradhi yanayoambatana na magonjwa ya moyo. Mnyumbulisho huu umeonyesha pia kwamba, watu wenye maradhi ya moyo na mfumo wa mishipa ya damu (cardiovascular diseases) waliokuwa wakifanya mazoezi mara kwa mara, walijikinga na vifo vya mapema vinavyoweza kusababishwa na maradhi hayo. Tafiti zinatuonyesha kwamba japo mazoezi hufanya kazi vizuri zaidi katika kuzuia magonjwa, mazoezi pia yana mchango mkubwa katika kuponya magonjwa hayo. 

Mazoezi ya kasi (aerobics) na ya nguvu (resistance) husaidia kuzuia ugonjwa wa kisukari

Matokeo ya utafiti mkubwa uliohusisha madaktari wa kiume takribani 21,000 huko nchini Marekani umebaini kuwa, asilimia kubwa ya madaktari waliokuwa wakifanya mazoezi ya kutosha kutoa jasho kila mara, hawakupata ugonjwa wa kisukari ukilinganisha na wale wasiofanya mazoezi. Mazoezi haya yalihusisha yale ya kasi (aerobics) na hata ya kutumia nguvu (resistance). Faida hizi chanya zilionekana zaidi katika kundi la watu wenye uzito mkubwa ambao kiuhalisia wanahatari kubwa zaidi ya kupatwa na ugonjwa huo. Hii inamaana kwamba mazoezi huweza kuzuia ugonjwa wa kisukari hata kwa watu wenye uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huo, ikiwamo wenye historia za tatizo hilo katika familia zao. Ziko tafiti nyingi zinazoshabihiana na utafiti huu. Mnyambulisho wa muunganisho wa matokeo ya tafiti nyingi katika eneo hili umeonyesha pia kwamba kwa kufanya mazoezi mara kwa mara na kula lishe bora, watu wenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari wanaweza kuzuia ugonjwa huo kwa asilimia hadi 60.

Huzuia saratani ya matiti na utumbo mpana

Mnyambulisho wa mkusanyiko wa matokeo ya tafiti zaidi ya 100 (meta-analysis) umeonyesha kwamba mazoezi ya wastani kama sehemu ya kazi, kusafiri au mazoezi maalumu huzuia saratani ya matiti na utumbo mpana kwa wanawake na wanaume. Matokeo haya yanaonyesha kwamba kufanya mazoezi hata kwa jumla ya saa mbili kwa wiki huleta faida hiyo. Mazoezi yaliyo sehemu za shughuli za kila siku ni kama vile kufanya usafi, kulima, kusukuma mashine na vitu vyote vinavyohusisha kujongea wakati wa kazi. Mazoezi yaliyo sehemu ya usafiri ni kutembea na kuendesha baiskeli wakati mazoezi maalumu huusisha michezo na kwenda gym.

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana naye kwa kutumia namba 0752255949, baruapepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea moja ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles