25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

MATIANG’I: MIGUNA SHARTI AOMBE TENA URAIA WA KENYA

NAIROBI, KENYA


WAZIRI wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Dk. Fred Matiang’i amesema mwanasiasa wa upinzani aliyetimuliwa nchini Kenya, Miguna Miguna atalazimika kuomba tena uraia.

Waziri huyo amesema Miguna alipoteza uraia wake alipochukua wa Canada mwaka 1988, hivyo hawezi kuruhusiwa kuingia Kenya kama raia bila kuomba tena uraia.

Dk. Matiang’i aliyekuwa akihojiwa na Kamati ya Bunge, amesema mwanasiasa huyo ambaye pia ni wakili alijipatia pasipoti na kitambulisho cha taifa anachokitumia sasa kwa njia ya ulaghai.

Waziri huyo amesema hakuna anayepinga Miguna alizaliwa Kenya.

“Yeyote aliyechukua uraia wa taifa lingine kabla ya Katiba ya sasa kuidhinishwa mwaka 2010, ambaye anafikiri anaweza kuitumia bila kufuata utaratibu uliowekwa anajidanganya.

“Hapana shaka Miguna alizaliwa Kenya. Lakini kwa mujibu wa Katiba ya kabla ya 2010, yeyote aliyechukua uraia wa nchi nyingine alipoteza uraia wa Kenya. Bunge liliidhinisha sheria inayoeleza jinsi mtu wa aina hiyo anavyoweza kupata tena uraia wake.” Alisema.

Waziri huyo pia alijitetea dhidi ya shutuma kuwa amekuwa akikaidi maagizo ya mahakama ya kutaka Miguna aachiwe huru na kuruhusiwa kuingia Kenya.

Jaji wa Mahakama Kuu, George Odunga alikuwa ameagiza Dk. Matiang’i, pamoja na Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet, Mkuu wa Uhamiaji Gordon Kihalangwa na Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Karanja Kibicho wafike mbele yake kueleza ni kwa nini walikaidi amri ya mahakama ya kumruhusu Miguna aingie Kenya.

Dk. Matiang’i amesema: “Jaji alipokuwa anatutaka tufike mbele yake tulikuwa tunahudhuria sherehe za kufuzu kwa maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU). Tulihukumiwa bila kupewa fursa ya kujieleza, kwa kutumia madai ya uongo,” alisema.

Jaji Odunga aliwapiga faini ya shilingi mia mbili kila mmoja na akaagiza pesa hizo zikatwe kutoka kwenye mishahara yao.

Dk. Matiang’i pia alipuuza madai kuwa serikali ilimfurusha Miguna kutoka Kenya akisema hatua kama hiyo ingehitaji idhini yake.

“Hakufurushwa kutoka Kenya. Nilihitaji kutia saini idhini ya kumfurusha. Hatungemfurusha kwani hakuwa ameingia bado ndani ya eneo la utawala wetu.

“Tulimuondoa uwanja wa ndege kama mtu ambaye hakuwa na nyaraka za kumtambua, abiria ambaye hangetambuliwa ambaye kawaida hurejeshwa alikotoka,” alisema Dk. Matiang’i.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles