Na FERDNANDA MBAMILA, DAR ES SALAAM
TOHARA kwa wanawake au ukeketaji ni taratibu zinazohusisha kuondolewa kabisa au kukata sekemu ya via vya uzazi vya mwanamke au uharibifu mwingine katika viungo vya uzazi kwa sababu zisizo za kitabibu.
Kati ya wanawake na wasichana zaidi ya milioni 100 duniani kote wamefanyiwa ukeketaji, wakiwemo milioni 92 katika Afrika.
Kitendo cha ukeketaji ni kinyume cha sheria na maadili ya nchi, lakini bila kujali vitendo hivyo bado vinafanywa kwa kiwango kikubwa vikiongozwa na Mangariba.
Kumkeketa mototo wa kike ni ukiukwaji wa haki za binadamu chini ya makubalianao ya haki ya mtoto.
Aidha, ukeketaji wa wanawake na wasichana ni ukiukwaji wa haki yao ya maisha ya afya njema ya kijinsia na ualisia wake.
Hapa nchini ukeketaji ulitangazwa kuwa ni kinyume cha sheria na kosa la jinai mwaka 1998 katika Sheria ya Makosa ya kujamiiana (SOSPA) ambayo ilifanyiwa marekebisho kanuni ya adhabu kama ifuatavyo.
Matatizo yanayotokana na ukeketaji
Kwa mujibu wa WHO matatizo yafuatayo mara nyingi huweza kutokea mara tu baada ya msichana au mwanamke kufanyiwa kitendo cha ukeketaji.
Licha ya maumivu makali anayoyapata baada ya kukeketwa, kwa kuwa anakuwa hana ganzi na dawa ya kupumguza maumivu kwa kawaida huwa haitumiki, ingawa wanawake na wasichana wengi hukabiliana na hatari hizi.
Baada ya kukeketwa tu msichana hutokwa na damu kupita kiasi, kupungua kwa damu mwilini, mshtuko, ugumu katika kupitisha mkojo na kinyesi, maambukizi ya magonjwa mbalimbali kama vile VVU lakini pia huweza kupoteza maisha.
Kwa mtu aliyefanyiwa ukeketaji ni rahisi kupata magonjwa makubwa ambayo ni sugu maishani kama vile uvimbe wa uke uliojaa maji (kufikia ukubwa wa mpira wa tenesi), kutosikia raha wakati wa kujamiana, uvimbe wa kisimi unaosababisha maumivu makali sana wakati wa kujisaidia.
Kutoka usaha katika sehenu ya nje ya uke na hiyo huweza kusababisha maambukizi wengine kwa urahisi wakati wa kufanya tendo, maambukizi ya kujirudia rudia katika njia ya mkojo, mivurugiko ya siku za hedhi na maambukizi ya kudumu katika nyonga yanayosababisha ugumba.
Ni muhimu kufikiria kwa umakini kuhusu nani ananufaika kifedha kutokana na ukeketaji na jinsi suala hilo linavyoendelea.