28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MATANUZI YA AJABU YA SULTAN WA BRUNEI

JOSEPH HIZA NA MTANDAO


NI mtawala wa kifalme wa taifa dogo lililopo katika Pwani ya Kaskazini mwa Kisiwa cha Borneo kilichopo Kusini Mashariki mwa Asia.

Brunei ni kisiwa kinachomilikiwa na familia ya kifalme kikiwa katika muundo wa meli ya kisultani.

Naam, Hassan al Bolkiah ni Sultan wa 29 na wa sasa wa taifa hilo linalofahamika kama nchi ndogo duniani, lakini moja ya mataifa tajiri.

Mapato yake hutokana na mauzo ya gesi na mafuta, kitu kinachomfanya Sultan kuishi kifahari, kwa amani na maisha ya peponi!

Mapema miaka ya 1990, Sultan alitangazwa kuwa mtu tajiri zaidi duniani kwa utajiri uliokadiriwa kuwa dola bilioni 40.

Kwa mujibu wa orodha iliyowekwa na Jarida la Time, Sultan pia alikuja kuwa mtawala wa pili wa kifalme duniani kwa utajiri wake wa dola bilioni 20 baada ya Mfalme wa Thailand Bhumibol Adulyade.

Utajiri wake uliongezeka kwa Euro 90 kila baada ya sekunde moja. Imetabiriwa kwamba kwa kiwango cha sasa. Mwanae wa kiume huenda akawa trilionea wa kwanza duniani miaka inayokuja.

Aidha, kufuatia kifo cha Mfalme wa Thailand, Bhumibol Adulyadej, mwaka 2016, Sultan Bolkiah akawa mtawala wa kifalme tajiri kuliko wote duniani.

Kadhalika, baada ya Malkia wa Uingereza, Elizabeth II, Sultan Bolkiah ndiye mtawala wa kifalme aliye madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani.

Oktoba 5, 2017, alisherehekea mwaka wake wa 50 tangu atawazwe kukalia kiti hicho cha enzi.

Kinachomtofautisha sultan huyu na viongozi wa kisiasa na hata watawala wengine wa kifalme duniani katika dunia hii ya kisasa ni kupenda kwake matanuzi kupita kiasi, mwepesi wa kutumia fedha bila huruma au kujiuliza mara mbilimbili.

Kwa maneno mengine, ana sanaa yake ya kutumbua fedha na kuendekeza staili yake ya maisha isiyo ya kawaida, ambayo daima imekuwa ikimulikwa na vyombo vya habari.

Unapopitia mali anazomiliki, ni kana kwamba utajiri wa Sultan unamnong’oneza kwa kumwambia: “Nitumie.”

Mkusanyiko wa magari yake 7,000 ni wa kila aina, ambao wapenda magari ya bei mbaya wasingependa kuyakosa.

Aina za magari ghali kabisa duniani: ikiwa ni pamoja na Rolls Royce 604, Mercedes-Benz 574, Ferrari 452, Bentley 382, Koenigsegg 134.

Mengine ni Lamborghini 21, Aston Martin 11, Jaguar 179 na BMW 209, ambapo yote kwa pamoja yana thamani ya dola 300,000,000 sawa na zaidi Sh bilioni 623.

Miongoni mwa gari hayo kuna lile la aina yake linalotumika kwa harusi lililonakishiwa kwa dhahabu ya uzito wa Carat 24 aina ya Rolls Royce lenye thamani ya dola milioni 14.

Hekalu lake rasmi linafahamika kama makazi makubwa kabisa ya kifamilia duniani.

Lina vyumba 1,788 bafu na vyoo 257, ukumbi wa sherehe wenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wageni 5000 na msikiti wenye uwezo wa kuchukua watu 1,500.

Hekalu hilo lina nafasi pana kwa ajili ya farasi wa mbio za farasai 200, gereji yenye uwezo wa kulaza magari 110 na mabwawa matano ya kuogelea.

Kama mtu akitaka kukagua kila chumba kwa sekunde 30 itamchukua saa 24 yaani siku moja nzima kukamilisha kazi hiyo.

Sultan huyo wa Brunei anamiliki ndege tatu binafsi za bei mbaya, ambazo zinaonekana kama jumbe la kifahari vile.

Ndege binafsi ya Sultan aina ya Boeing 747-400 ina sebule, chumba cha kulala na sinki zake ni dhahabu tupu.

Imekorombezwa na vitu vya kisasa na kunakishiwa na dhahabu safi kwa vile Sultan mwenyewe anaishi na kuogelea katika bahari ya dhahabu.

Kama hiyo haitoshi, ndege hiyo imegharimu dola milioni 520. Pia ana ndege ndogo sita na helikopta mbili.

Ndege ya Boeing 767 inaweza kuchukua abiria katika madaraja matatu. Humruhusu Sultan kusafiri kutoka Brunei kwenda Ulaya au Marekani bila kusimama.

Sultan alimpa zawadi kaka yake jumba kubwa la kifahari huko Las Vegas, Marekani lenye thamani ya dola milioni 60 likiwa na vyumba 92, vyumba vya kulala 29 Bafu 42 likiwa limetanda katika eneo la ukubwa wa futi mraba 108,895. Bila kusahau kiwanja cha tennis, mabwawa matatu ya kuogelea na gereji kubwa.

Harusi za kifahari za binti na mwanae ziliripotiwa kudumu kwa zaidi ya wiki moja.

Harusi hixzo zinakadiriwa kumgharimu Sultan dola milioni 15 hadi 20 kila moja, kitu ambacho ni suala dogo sana kwake.

Mke wa mwanae alivalia viatu vya mchuchumio ghali zaidi duniani pamoja na kikuku cha dhahabu safi. Ni sawa kabisa kusema kwamba harusi hizo zilifanyika katika bahari ya dhahabu.

Kampuni ya Kimataifa ya Asprey International Limited inafahamika kwa sifa yake ya kubuni, kutengeneza na kusambaza bidhaa za dhahabu, fedha na almasi kwa watawala wa kifalme kote duniani.

Sultan huyu asiyejua maana ya ubahiri, kazi yake kubwa kutumbua fedha tu, hununua vito kwa familia yake vyenye thamani ya dola milioni 17 kwa mwaka.

Kwa sababu hiyo, kama hiyo haitoshi akajiuliza kwanini asiinune kabisa kampuni hiyo? Nini cha kumzuia? Hakuna! Akamwaga dola milioni 385 mwaka 1995 kuinunua kampuni hiyo nzima ili kutosheleza mahitaji na ‘kiu’ yake inayotulizwa na dhahabu.

Wakati wa harusi ya kifalme ya Princess Rashidah, Mwimbaji mashuhuri wa Mareakani wa mahadhi ya R&B, marehemu Whitney Houston alikaribishwa kutumbuiza.

Aliripotiwa kulipwa dola milioni saba kwa shoo ambayo inahesabiwa kuwa ya nadra kutokea.

Harusi hiyo ya kumwaga, ilidumu kwa wiki mbili na kumgharimu dola miliioni 27 ambapo Prince Charles wa Uingereza alikaribishwa.

Aidha, Sultan aliripotiwa kumlipa mwanamuziki mwingine mashuhuri wa Marekani, mfalme wa Pop marehemu Michael Jackson dola milioni 17 kwa matamasha matatu moja likiwa kwa ajili ya wageni 6,000 na mawili kwa wageni binafsi wa Sultan.

Sultan pia hutumia si chini ya dola 25,000 sawa na Sh milioni 60 kunyoa nywele zake na huhakikisha kinyozi wake anayekuja na kuondoka kumnyoa anapanda ndege ya kifahari na salama inayomgharimu dola 18,000 sawa na Sh milioni 38.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles