Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MSAIDIZI wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Juma Matandika na Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Martin Chacha, wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh milioni 25.
Washtakiwa hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai washtakiwa walitenda makosa hayo Februari 4, mwaka huu.
“Mheshimiwa Hakimu washtakiwa Matandika na Chacha, wanashtakiwa kwa kosa moja la kuomba rushwa kinyume cha sheria ya kuzuia rushwa.
“Washtakiwa mnadaiwa Februari 4 mwaka huu, mkiwa waajiriwa wa TFF katika makao makuu yake, mlishawishi kuomba rushwa ya Sh milioni 25 kutoka kwa Salum Kulunge na Constantine Morandi.
“Kulunge na Morandi ni maofisa kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita na Klabu ya Mpira wa Miguu Geita.
“Washtakiwa mliwaomba rushwa kama kishawishi kwa TFF na Idara ya Uhamiaji Tanzania, kutoa uamuzi dhidi ya Klabu ya Mpira wa Miguu Polisi Tabora, ili kuisadia Klabu ya Geita kupanda katika Ligi Kuu Tanzania,” alidai Swai.
Baada ya kusomewa mashtaka, washtakiwa walikana kutenda makosa hayo, upelelezi wa kesi umekamilika.
Swai aliomba kesi ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Hata hivyo, mahakama ilikubali kuwapa dhamana washtakiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili, wenye barua na vitambulisho watakaosaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni tano kila mmoja.
Washtakiwa wametimiza masharti ya dhamana na wako nje hadi Novemba 30 mwaka huu, kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.