*Serikali yakusudia kupitia upya bei ya vitalu vya uwindaji
Na Kulwa Karedia
VITA ya utumbuaji majipu iliyoanzishwa na Rais Dk. John Magufuli tangu alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana, inazidi kushika kasi, baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, kusema wakati wowote kuanzia sasa Serikali itaanza mchakato wa kupitia upya bei ya umiliki wa vitalu vya uwindaji, ili kuona kama inakidhi vigezo.
Akizungumza na MTANZANIA jana kuhusu mikakati mbalimbali ya wizara yake, Profesa Maghembe alisema eneo la vitalu limekuwa na malalamiko mengi ambayo yanapaswa kushughulikiwa.
“Moja ya mkakati mzito niliona nao hivi sasa, nikupitia upya bei za umiliki wa vitalu vya uwindaji…eneo hili limekuwa likilalamikiwa mno na watu kwamba wapo wajanja wanja ambao wanalipa fedha kidogo.
“Kutokana na umuhimu na uzito wa rasilimali za Taifa hili, hatutakubali kuona zinashindwa kunufaisha Watanzania wote…tuko tayari kupambana usiku na mchana kulinda viumbe hivi ambavyo tumepewa na Mungu.
“Miaka 10 iliyopita nilikuwa kwenye wizara hii nikatoka, wakati huo nakumbuka kuna vitalu vilikuwa dola za Marekani 30,000 na kulikuwa na watu wanne au watano wanamiliki kilomita 2,000, lakini wanalipa fedha kidogo.
“Nakuomba uwe na subira ndiyo kwanza nina wiki moja sasa wizarani…nitakutana na timu yangu, tutapitia maeneo yote kuona kama kuna kasoro,”alisema Waziri Maghembe.
Lakini takwimu zinaonesha bei ya sasa ya vitalu vya uwindaji ambavyo vimegawanywa katika madaraja matatu, ni kwamba daraja la kwanza ni Dola za Marekeni 60,000 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.38, darala ja pili Dola 30,000 sawa na zaidi ya Sh milioni 690 na daraja la tatu, Dola 18,000 (zaidi ya Sh milioni 41).
Alisema mkakati wa pili ni kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa magogo na uharibifu wa misitu ambao sasa unaelekea kusababisha nchi kugeuka jangwa.
“Kwanza nikuhakikishie kuwa ni marufuku kusafirisha magogo, hapa lazima tuendelee kuwa wakali.. tukiwa wapole tabia hii ndiyo inasababisha misitu yetu inakatwa kila kukicha, vyanzo vya maji vinaelekea kutoweka… sasa hivi ukitembelea maeneo mengi ya mito yetu inaelekea kukauka kwa sababu ya uharibifu wa mazingira.
“Tutatumia sheria zetu ipasavyo kupambana na uhalifu huu ambao haukubaliki hata kidogo, kila mmoja atakayebainika hatua kali zitachukuliwa haiwezekani kila siku tuimbe wimbo huo huo tu,”alisema.
Alisema kuruhusu kuendeleza biashara hiyo, ni kutaka kuiweka Tanzania katika mazingira magumu, jambo ambalo alisema halitavumiliwa.
Profesa Maghembe alisema mkakati wake wa tatu, ni kuhakikisha kunakuwapo na ongezeko kubwa la hoteli za kitalii.
“Tunahitaji kuwa na hoteli nyingi za kitalii ambazo zitaweza kubeba wageni wa kimataifa…mkakati huu utasaidia Taifa kuongeza pato la kigeni.
“Tuna mbunga nyingi ambazo naamini kama tukifanikiwa kuwa hoteli nyingi na kuzitangaza ipasavyo ni wazi hata wale washindani wetu tutawaacha mbali…uwezo huu tunao,”alisema Waziri Maghembe.