25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mataifa makubwa yasaini kutoingiza silaha Libya

Berlin, Ujerumani

VIONGOZI wa dunia wamejitolea kutafuta namna ya kuzuia mataifa mengine kuingilia katika vita nchini Libya.

Pamoja na hilo wameazimia kuzingatia marufuku ya silaha nchini humo.

Hayo yamefikiwa katika mkutano ulioandaliwa mjini Berlin  kuhusu kukomesha mzozo nchini humo.

Marais wa Urusi, Uturuki na Ufaransa, walikuwa miongoni mwa viongozi wa kimataifa waliotia saini makubaliano hayo ya kusitisha uingiliaji wa vita hivyo aidha kupitia kuepeleka silaha, vikosi vya kijesi ama ufadhili.

Wakati viongozi wa mataifa hayo makubwa wakikubaliana hayo, hali ilikuwa ni tofauti kwa pande zinazozozana nchini humo.

Mazungumzo hayo yalishindwa kuleta maridhiano kamili kati ya pande zinazozozana za kamanda muasi Khalifa Haftar na mkuu wa serikali inayotambulika na Umoja wa Mataifa Fayez al-Sarraj.

Kutokana na hatua hiyo pande hizo mbili zilishindwa kutia saini mkataba wa kudumu wa kusitisha mapigano.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema kuwa hali ya Libya ni tete kwamba ni vigumu  kuhakikisha usitishaji wa mara moja wa mashambulizi unazingatiwa.

Lakini alisema ana matumaini kwamba kupitia mkutano huo, fursa ya mpango huo unaweza kudumishwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, amethibitisha kuwa ”bado kuna maswali kuhusu jinsi ya kushughulikia kikamilifu” na kufuatilia kujitolea huko.

Lakini amesema kuwa ana matumaini kwamba kutakuwa na ghasia za kiwango kidogo.

Mjumbe maalumu, Ghassan Salame amekuwa akijaribu kuendeleza fursa ya kuanza mazungumzo kati ya pande zinazozozana nchini Libya.

Libya imegawika kati ya pande mbili pinzani tangu vuguvugu la mwaka 2011 lililoungwa mkono na jumuiya ya kujihami ya NATO lilipomuuwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gadhafi.

Katika siku za hivi majuzi, vikosi vinavyoongozwa na Sarraj mjini Tripoli, vimekuwa chini ya mashambulizi tangu mwezi Aprili kutoka kwa vikosi vinavoongozwa na Haftar.

Mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya raia 280 na wapiganaji 2,000 huku maelfu ya watu wakipoteza makazi yao.

Hali hiyo ilishuhudiwa hadi pale mkataba hafifu wa kusitisha mapigano unaoungwa mkono na Uturuki na Urusi ulipowekwa tarehe 12 mwezi Januari.

Japokuwa Serikali ya Sarraj inatambuliwa na Umoja wa Mataifa, mataifa yenye ushawishi mkubwa yamejitenga na kumuunga mkono Haftar na kuugeuza mzozo wa taifa hilo kuwa kile ambacho baadhi wamekitaja kuwa vita kubwa ambapo mataifa ya kigeni yameingilia kulinda maslahi yao.

Wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya jana walikuwa wakizungumzia hatua zitakazofuata katika kutekeleza harakati za amani zilizokubaliwa wakati wa mkutano huo mjini Berlin.

Kabla ya mkutano huo, Umoja wa Ulaya uliahidi kufanya kila linalowezekana kutekeleza makubaliano yoyote yaliyoafikiwa katika meza ya mazungumzo hasa kuhusiana na hatua ya kusitishwa kwa mapigano na marufuku ya silaha ya Umoja wa Mataifa kwa Libya.

Mkuu wa Sera za Kimatifa wa Muungano huo, Joseph Borell amesema hatua hiyo ni njia ya kutuma ujumbe wa Muungano wa Ulaya katika taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika. Ugiriki na Italia tayari imeonyesha kujitolea kwake kupeleka vikosi vya kijeshi huku Ujerumani ikisema inakadiria iwapo itashiriki katika hatua hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles