Na SWAGGAZ RIPOTA
YAKIWA ni maadhimisho ya 107 ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, nyota mbalimbali kutoka kwenye kiwanda cha burudani nchini na nje ya mipaka ya nchi yetu, Alhamisi wiki hii waliungana na mastaa ulimwenguni kote kuiadhimisha.
Mastaa hao wamekuwa gumzo kwa maneno yao yenye kutia moyo, kuibua ari mpya na kuonyesha thamani ya mwanamke.
Zifuatazo ni jumbe zenye nguvu zilizonogesha siku hiyo, ambazo Swaggaz tumezinasa kutoka kwa mastaa mbalimbali duniani kutoka sekta ya burudani.
Wa kwanza kabisa ni Emmanuel Mbasha, mwimbaji wa muziki wa Injili ambaye ametumia siku hiyo kumuomba aliyekuwa mkewe, Flora mtoto wao Lizy.
EMMANUEL MBASHA
“Ulinizalia mtoto mzuri sana kwa hilo nakushukuru mno, nimem-miss sana Lizy sasa unipage basi mtoto, unaninyima kabisa karibu mwaka wa pili inaelekea wa tatu sijamwona mtoto.
“Miye baba yake tu ila nakuomba hata siku moja moja nifurahie maisha na dogo, nakuomba nimwone mwanangu Lizy, najua hata mtoto ameni-miss maana ameondoka kwangu akiwa mkubwa na nimemlea tangu mtoto ila anashindwa kuongea tu ila najua ananikumbuka sana.
“Mahakama iliamua mtoto akae na mama ila niwe namwona, sasa unapingana na mahakama. Nimeongea na mzazi mwenzangu x wife, mke wa mtu – njia za kawaida naona imeshindikana sasa inabidi nikuombe Insta,” anasema Mbasha kupitia ukurasa wake wa Insta.
JOKATE
Staa huyu ambaye siku hiyo alitambulisha bidhaa yake ya begi za Kidoti kwa ajili ya mwanafunzi kubebea daftari alisema: “Lil Kidoti ni binti mwenye ndoto kubwa za kufanikiwa kwenye maisha, haamini katika kuzuiliwa na kitu chochote anaamini jamii itaondoa ndoa za utotoni na vikwazo vyote ambavyo pengine vitakwamisha ndoto zake.
“Anaamini jamii itahakikisha ana haki ya kuwa na maamuzi na mchango kwenye masuala yote yanayomhusu yeye na jamii yake iwe kisiasa, kiuchumi, kiafya, kijamii, ataongea, atasikilizwa na ataingia kwenye vitabu vya historia. Je wangapi wapo kama Lil Kidoti?”
OPRAH WINFREY
Huyu ni mtangazaji wa kike mwenye ushawishi mkubwa duniani kutoka nchini Marekani, yeye alisema: “Kazi yenu pekee duniani, watu wanafikiri kazi yenu ni kulea familia. Ndiyo, hilo ni jukumu lakini jukumu lenu kubwa ni kutambua kilichowaleta duniani.”
BATULI
Anasema: “Nguvu yetu haina mfano katika dunia, wingi wetu huonyesha wazi sisi ndiyo wenye dunia
tunapatikana kila mahala na tukikosekana mambo hayaendi sawa, hakuna nyumba inakosa mwanamke ila zipo nyumba hazina wanaume.”
RAYVANNY
Anasema: “Hata kama ulitengana na mama yako au haujawahi kumwona au yupo na wewe au kashatangulia mbele ya haki, amini kuwa upendo wa mama haufutiki, dua zake ndiyo mafanikio yako, heshimu kila mwanamke, huyo ni mama kama siyo mama yako ni mama wa mwanao.”
WEMA SEPETU
Anasema: “Siku ya wanawake duniani mimi napenda kumpa ufahari zaidi mwanamke aliyenileta duniani, mama yangu ndiyo mwanzilishi wa maisha yangu, mama ni nguzo, mama ni tegemeo la kila mwanadamu.
“Ukitaka kunijua side B yangu basi nitafute kwa mama yangu, utaniona mbaya, mzazi mwenyewe ninaye mmoja tu ndo’ aliyebaki, kwanini nisimthamini na kumpigania?”
BEYONCE
Staa huyu ambaye ni wa muziki duniani amewapa ujumbe mzuri wasichana na wanawake kwa kusema: “Tunatakiwa kuhifadhi miili yetu na tunachokitumia kuihifadhi. Wanawake tunapaswa kutumia muda wetu kuangalia afya na imani zetu bila kuwa wabaguzi. Tambua, ulimwengu utakuchukulia jinsi ulivyo.”
ZARI THE BOSS LADY
“Ndiyo, nazungumza na wewe, uliye hapo. Wewe ni mwanamke wa kweli. Hebu ‘wa-tag’ wenzako wa ukweli. Naanza na mimi, niko hapa, Mimi ni mwanamke wa nguvu. Nawatakia siku njema ya Wanawake.”