25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mashine za BVR zakwamisha uandikishaji

Waandishi Wetu – Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Wilson Mahera,  amesema uandikishaji wa wapiga kura ulianza kwa kusuasua kwa siku mbili katika baadhi ya maeneo kutokana na mshine za BVR kuwa na hitilafu za ufundi,  ambapo sasa zimerekebishwa.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk, Mahera, alisema kuwa yeye na wasaidizi wake walipata taarifa ya hitilafu hizo juzi na hivyo kuanza kuzunguka sehemu nyingi na kufanya marekebish ambapo kwa siku ya jana kazi ya uandikishaji iliendelea vizuri.

Alikuwa akitoa ufafanuzi wa suala hilo baada ya gazeti hili litaka kujua hatua zilizochukuliwa na NEC kutokana na ufanisi mdogo wa mashine za BVR ambazo zilianza kutumia vituoni tangu Ijumaa Februari 14, ambapo NEC ilianza uandikishaji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

“Ni kweli jana na juzi (Ijumaa na Jumamosi) kulikuwa na jambo kama hilo lakini sasa zimekaa sawa. Unajua sasa hivi hizi mashine zimefanya kazi mikoa 24 na hivi sasa tunamalizia Pwani na Dar es Salaam hatukupata muda wa kuzifanyia matengenezo lakini baada ya changamoto za juzi na jana tuimepata muda wa  kuzifanyia makerekebisho.

“Jana kulikuwa na changamoto ya printer (mashine za kuchapia), sana sana ndizo ambazo zimeleta changamoto na kweli iliathiri kidogo lakini baada ya kuingilia kati jana (juzi)  na leo (jana) ninaendelea kupokea taarifa hapa.

“Pwani yote kuna wataalamu wangu wanazunguka, mimi mwenyewe leo (jana) nimezunguka nimekwenda Kinondoni na Oysterbay huku mashine zinakwenda vizuri, kuna watu wako Temeke na wengine saa hivi Chalinze ninapata taarifa kuwa hali ni nzuri,” alisema Dk. Mahera

Alisema hadi sasa wako katika hali ya tahadhari na kama kuna sehemu ina tatizo basi inawezekana kuna changamoto ndogo siyo kubwa na itatatuliwa.

“Ila ni kweli zilikuwepo changamoto kweli kwa sababu tulianza juzi (Ijumaa), jana (Jumamosi) zile mashine zimefanyiwa ukarabati na ilikuwa ni changamoto ambayo walichelewa tu kuripoti, kwa maana mashine tunazo za kutosha. Walishindwa kuripoti mapema,” alisema

Alisisitiza kuwa tayari ameshatoa maelekezo wataalamu wa NEC wanazunguka na makamishna wa tume hiyo  wanazunguka kwa hiyo wanaendelea kupokea taarifa zao kila wanapokwenda na ikitokea changamoto wanatatua.

“Tumeanza kwa kusuasua lakini tunaendeela kuboresha uandikishaji. Watu leo (jana) ni wengi wanajitokeza, labda changamoto nyingine niliyoiona kuna maeneo yenye watu wengi zimepelekwa mashine chache na mengine yana watu wachache zimepelekwa nyingi, ni suala ambalo tunalishughulikia,” alisema.

HALI VITUO

Alisema ana imani kufikia leo watu watajitokeza zaidi kwa sababu siku waliyoanza kuandikisha ilikuwa ni siku ya Valentine na ikafuata wikiendi, hivyo anadhani kuanzia leo Jumatatu watajitokeza wengi zaidi.

Alisema anaona mwitikio ni mkubwa katika maeneno ambayo wamepitia na wanawaomba wananchi wajitokeze kwenye vituo ambavyo wameviweka kwenye shule za msingi, sekondari na kwenye ofisi za kata na za Serikali za Mitaa waende wakajiandikishe na kuboresha taarifa zao.

Alisema watambue kuwa kadi yao ndiyo kura yao na ndiyo maendeleo yao na kwa kupiga kura ndipo unapoweza kuchatgua kiongozi ambaye unaamini mtasaidiana kuleta maendeleo, ni mmuda mfupi tu haichukui muda mrefu.

MTANZANIA ilitembelea katika baadhi ya vituo na kuzungumza na wenyeviti wa Serikali za Mitaa jijini Dar es Salaam ambapo  walisema uandikishaji unaendelea vizuri japokuwa changamoto kubwa ni kuharibika kwa mashine za BVR.

Wenyeviti hao walisema mashine hizo zimekuwa zikisumbua na kusababisha uandishaji kusuasua.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mongolandege, Kata ya Ukonga Manispaa Ilala, Rajab Tego (CCM), alisema katika mtaa huo kuna vituo viwili vya kujiandikisha huku mashine moja ikisumbua na kusababisha usumbufu kwa wananchi waliofika kujiandikisha.

“Jana (juzi) mashine moja iliharibika siku nzima na kusababisha uandikishaji kuzorota lakini leo (jana) imeanza kufanyakazi na sasa tuendelea vizuri,” alisema Tego.

Naye Mwenyekiti wa Sinza E, Kata ya Sinza Manispaa ya Ubungo, Keneth Kavishe alisema mtaa huo una vituo vitatu na mashine tatu kati ya mashine hizo moja iliharibika.

“Mashine moja iliyopo Kituo cha Queen of Sheba ilikuwa mbovu tuliwapigia wataalamu wa IT wameahidi kuja kuichukua,” alisema Kavishe.

Alisema idadi ya watu wanaojitokeza kujiandikisha kwa sasa ni wachache kutokana na matangazo kutokuwafikia wengi.

Naye Mwenyekiti wa Sinza D, Muumini Herezi alisema wameamua kuitisha mkutano kuwahamasisha wananchi waweze kujitokeza katika uboreshaji wa daftari hilo.

“Wananchi wanaojitokeza ni wachache ukilinganisha na idadi ya wakazi wa mtaa huu hivyo asubuhi (jana) tuliitisha mkutano wa wajumbe wa mashina wakawahamasishe wananchi,” alisema Herezi.

Alisema kwa siku mbili wameweza kuandikisha wapigakura 600 tu japokuwa wanaotakiwa kujiandikisha ni waliopoteza vitambulisho, vilivyochakaa, waliohamia na vijana ambao ndio wanatimiza umri wa kujiandikisha.

TAARIFA YA NEC

Katika taarifa yake awali, kuhusu uboreshaji wa daftari hilo, NEC ilisema uandikishaji ajili ya uboreshaji wa taarifa za daftari la kudumu la wapiga kura utafanyika kwa katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa siku saba, kuanzia Februari 14 hadi 20 mwaka huu.

Uboreshaji huo utafanyika katika vituo vilivyoko katika mitaa na vijiji kweney kata zote za mikoa hiyo, ambao utahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania kwa mujibu wa sheria watakaokuwa na umri wa miaka 18 na zaidi na wale watakaotimiza umri wa miaka 18 siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Wengine ni wapiga kura wenye kadi ya mpiga kura ya zamani iliyoharibika, wale wenye sifa lakini hawakujiandikiha mwaka 2015 na wale waliohama maeneo ambao wanatakiwa kuboresha taarifa zao katika maeneo yao mapya.

Habari hii imeandaliwa na Andrew Msechu, Christina Gauluhanga na Tunu Nassor

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles