31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA MWENDO WA KUWAGONGA TU

NA JESSCA NANGAWE

SIMBA imeendelea kujitengenezea mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli, katika pambano lililochezwa Uwanja wa Samora, Iringa.  

Mshambuliaji John Bocco ndiye aliyeipa Simba pointi tatu katika mchezo wa jana, baada ya kufunga bao pekee la Wekundu hao dakika ya 23.

Bocco alifunga bao hilo ambalo ni la tatu kwa upande wake msimu huu, baada ya kupokea pasi murua ya Fransis Kahata.

Kwa ushindi wa jana Simba imefikkisha pointi 56, baada ya kushuka dimbani mara 22, ikishinda michezo 18, sare mbili na kupoteza mara mbili.

Baada ya kichapo cha jana, Lipuli imeshuka kwa nafasi moja ikitoka ile ya tisa hadi ya 10, baada ya kucheza michezo 22, ikishinda nane, sare tano na kupoteza tisa hivyo kujikusanyia pointi 29.

Mchezo huo ulianza kwa kasi na kila timu kuonekana kudhamiria kupata mabao ya haraka.

Hatua hiyo ilisababisha kuwapo kwa kosa kosa tangu mwanzoni mwa mchezo, zilizotokea kila upande.

Dakika ya saba, mshambuliaji na nahodha wa Lipuli jana, Daruwesh Saliboko alishindwa kupachika bao kutokana na kutojpanga vema.

Dakika ya tisa, kipa wa Simba, Aishi Manula alipangua mchomo wa Kennedy Masumbuko.

Dakika ya 12, kipa wa Lipuli, Deogratias Munishi ‘Dida’ aliokoa mpira wa kichwa uliopigwa na mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere.

Dakika ya 31, beki wa Lipuli Paul Ngalema alionywa kwa kadi ya njano kutokana na kupinga uamuzi wa mwamuzi.

Kipindi kila upande ulijaribu kuzichanga karata zake, Lipuli ikitaka kusawazisha kabla ya kuongeza na Simba ikitaka kufunga mabao zaidi.


Hata hivyo, safu za ulinzi za kila upande zilifanya kazi nzuri kuepusha madhara langoni mwao na kufanya dakika 90 za patashika hiyo kumalizika kwa Simba kutakata kwa bao 1-0.

Kikosi cha Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Cloutas Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Francis Kahata.

Kikosi cha Lipuli: Deogratius Munishi, Duchu, Paul Ngalema, Mwassa, Mwangosi,Lufunga, Mwinyi,Tangalu, Joshua, Daruesh Saliboko, na Kennedy Masumbuko.

Michezo mingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana,  Azam ilijikuta ikiendelea kuwa mteja wa Coastal Union, baada ya kucharazwa mabao 2-1, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ikumbukwe kuwa, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kati ya timu hizo uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Coastal ambayo ilikuwa mwenyeji ilishinda bao 1-0. 

Mabao ya Coastal yalifungwa na Ayoub Lyanga na Mudathir Khamis.

Kwa mtokeo hayo, Coastal imepanda hadi nafasi ya nne, ikitoka ile ya sita ya awali, baada ya kufikisha pointi 37.

Bao la Azam lilipachikwa na dakika ya 90 na mshambuliaji, Obrey Chirwa.

Hata  hivyo, Azam inayofundishwa na kocha Mromania Aristica Cioaba, imesalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikiwa imejikusanyia pointi 44.

Kagera Sugar iliiadhibu Mbao mabao 2-0, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Mabao ya Kagera Sugar yaliwekwa kimiani na Yusuph Muhilu na Godfrey Mwashiuya.

Mhilu amefikisha mabao 10 msimu huu na kumkaribia Kagere anayekamata  uongozi akiwa na mabao 12.

Polisi Tanzania iling’ara baada ya kuitandika KMC mabao 3-2, huku Singida ikilazwa bao 1-0 na Ndanda na kuzidi kujiweka kwenye mazingira hatarishi zaidi ya kushuka daraja.

Nao Maafande wa Ruvu Shooting wakatakata bao 1-0 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Mwadui na Namungo zikagawana pointi moja moja baada ya sare yao ya bao 1-1 Uwanja wa Kambarage.

Mtibwa iliendelea kudorora baada ya kutandikwa bao 1-0 na  ya JKT Tanzania huku Biashara ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Alliance, Uwanja wa Karume, Mara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles