*Ni mchezo wa Azam kuchezewa Mwanza
Na Shomari Binda, Musoma
MASHABIKI wa timu ya Biashara United wamekilalamikia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kwa kushindwa kurekebisha uwanja wa kumbukumbu ya Karume kwa wakati na kusababisha mchezo wa Biashara na Azam FC kuchezewa jijini Mwanza.
Wakizungumza na Mtanzania Digital kwa nyakati tofauti, mashabiki hao wamesema ni uzembe wa viongozi kutokufatilia marekebisho ya uwanja hatua ambayo imechangia mchezo huo kuchezewa uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Wamesema tangu kumalizika kwa sherehe za miaka 45 ya CCM Februari 5, kulikuwa na muda wa kufanya marekebisho lakini wameshindwa kufanya hivyo.
Mmoja wa mashabiki hao aliyejitambulisha kwa jina la Juma Warioba, amesema wao kama mashabiki wameumizwa na jambo hilo na wanawalaumu viongozi wanaousimamia.
Amesema timu inapoutumia uwanja inapata asilimia 15 ya mapato lakini kufanya marekebisho inakuwa shida.
“Hawa viongozi wa CCM Mkoa wa Mara ambao ndio wasimamizi wa uwanja ni tatizo na hawajui masuala ya michezo. Tangu kumalizika kwa sherehe za CCM kulikuwa na muda wa kurekebisha uwanja timu yetu ikaendelea kuutumia lakini sasa wanatupa gharama za kwenda Mwanza,” amesema Juma.
Mtanzania Digital ilifanya juhudi ya kumtafuta katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Langaeli Akyoo, ili kuweza kuzungumzia marekebisho ya uwanja huo na kuendelea kutumika lakini simu yake iliita pasipo kupokelewa..
Biashara United ndio mwenyeji wa mchezo dhidi ya Azam Fc uliokuwa uchezwe kesho kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume mjini Musoma na sasa utachezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.