30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

MASAMAKI WA TRA HURU

*Wenzake watano wasomewa mashtaka 110, yapo uhujumu uchumi na utakatishaji fedha


NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki na wenzake wanne waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7, wameachiwa huru.

Wakati washtakiwa hao wakiachiwa huru, wenzao watatu wamesomewa mashtaka 110, yakiwamo utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Mbali na washtakiwa hao watatu ambao ni kati ya wanane walioshtakiwa na kina Masamaki awali, wengine wawili wameongezwa kwenye kesi hiyo jana na kuunganishwa kwenye mashtaka hayo.

Mashtaka mengine waliyosema ni pamoja na kufuta taarifa kwenye kanzi data (data base) kinyume cha sheria ya mtandao, kughushi, kutakatisha fedha, kusababisha hasara ya Sh bilioni 12.7 na kusaidia ukwepaji wa kodi wa kiasi hicho cha fedha.

 

MASAMAKI ALIVYOACHIWA

Jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, iliwaachia Masamaki na wenzake baada ya Wakili wa Serikali  Mkuu, Timon Vitalis kuomba waachiwe huru chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.

Wengine walioachiwa huru, ni Meneja Kitengo cha Huduma za Ushuru TRA, Habib Mponezya (45), Meneja Msimamizi na Ufuatiliaji wa Forodha, Burton Mponezya (51), Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha – bandari kavu ya Azam (AICD), Eliachi Mrema (31) na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan (59).

 

WANAOENDELEA NA KESI

Washtakiwa wanaoendelea na kesi mpya, ni Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Hamis Omary (48), Meneja wa Operesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Adolf Louis (39) na Haruni Mpande (28) wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta (ICT) TRA ambao wamesomewa mashtaka mapya 110 na wenzao wawili.

Washtakiwa wapya waliounganishwa nao jana na kusomewa mashtaka hayo ni Khalid Yusufu Louis ambaye ni mfanyakazi wa Azam na Benson Malembo, mfanyakazi wa Region Cargo Services. Walisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis mbele ya Hakimu Shaidi.

 

KESI MPYA

Katika kesi hiyo mpya, Haruni anadaiwa kuwa kati ya Julai 11 na Oktoba 28, 2015 Dar es Salaam, kwa makusudi alifuta taarifa katika kanzi data zinazohusu makontena 329 yaliyoingizwa nchini na kupelekwa katika bandari kavu ya Azam.

Kwa upande wa washtakiwa Raymond na Khalid, wao wanakabiliwa na mashtaka 105 ya kughushi hati 105 za kutoa makontena kwenye bandari kavu ya Azam iliyopo maeneo ya Sokota na kujaribu kuonesha yalitolewa kihalali na TRA Dar es Salaam.

Washtakiwa Raymond, Khalid, Haruni, Khamis na Benson, wanadaiwa kuwa kati ya Julai 11 na Oktoba 28, 2015 kwa vitendo vyao walisababisha hasara ya Sh bilioni 12.7 kwa kutoa makontena 329 bila ya kulipia ushuru na malipo mengine.

Mshtakiwa Raymond anadaiwa kutakatisha fedha, kati ya Julai 11 na 12, 2015  katika Benki ya CRDB tawi la Lumumba kwa kujihusisha na muamala wa Sh milioni 686.868 alizopokea kupitia akaunti yake namba 01J200754200 kutoka Kampuni ya XL  Clearing and Forwarding Ltd yenye akaunti namba 004120328300001 iliyopo Benki ya Amana wakati akijua ni zao la ukwepaji kodi.

Vitalis alidai Hamisi alitakatisha fedha kwa kijihusisha na muamala wa Sh milioni 25 ambazo alipokea kupitia akaunti namba 01J2026217700 kutoka kwa Sapato Kyando na washtakiwa wote wanadaiwa kusaidia ukwepaji kodi wa zaidi ya Sh bilioni 12.

Alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, watawasilisha taarifa kuhusu kesi hiyo Mahakama Kuu na Julai 27, mwaka huu watawasomea washtakiwa ushahidi.

Washtakiwa katika kesi hiyo wanatetewa na Wakili Nehemia Nkoko na Wakili Mashaka Ngole.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Julai 27 na washtakiwa walirudi rumande isipokuwa Haruni ambaye yuko nje kwa dhamana.

 

MASHTAKA YA AKINA MASAMAKI

Akina Masamaki walikuwa wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 17, 2015 walikula njama kwa kuidanganya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Sh bilioni 12.7.

Washtakiwa hao waliokuwa wanadaiwa kudanganya kuwa makontena 329  yaliyokuwapo katika bandari kavu ya Azam yalitolewa baada ya kodi zote kulipwa wakati wakijua si kweli.

Katika shtaka la pili, walikuwa wakidaiwa  kuwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao  na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.

 

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Ni vyema serikali na vyombo vyake vikabadili mfumo wa ukamataji washukiwa hasa pale panapokuwa hamna udharura wowote.
    Haipendezi na ni fedheha kumkamata mtu bila ya kuwa na ushahidi ambao mwisho wa siku unaifanya serikali kuonekana kutokuwa makini na yenye nia ovu!
    Jitafakarini!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles