WAIMBAJI nyota wa muziki wa Injili hapa nchini, Martha Mwaipaja, Jesca BM na Christopher Mwahangila, wanatarajia kupanda katika jukwaa la Tamasha la Krismasi linalotarajiwa kufanyika Desemba 25, kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Waimbaji hao wanaungana na wenzao waliotangulia kuthibitisha kushiriki tamasha hilo, ambalo lina malengo ya
kurudisha shukrani kwa Mungu baada ya kufanikisha uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 kwa amani na utulivu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, aliwataja wengine ambao watakuwa sambamba
na wenzao siku hiyo ni pamoja na Sifael Mwabuka sambamba na Kwaya ya Yombo KKKT.
Msama alisema tamasha hilo linadhaminiwa na gazeti la Dira ya Mtanzania, ambako alitoa wito kwa mashirika na kampuni mbalimbali kujitokeza ili kufanikisha tamasha hilo.
Aidha Msama aliwataja wengine waliothibitisha kupanda jukwaa la tamasha hilo ni pamoja na Rebeca Malope, Eiphraim Sekeleti, Solomon Mukubwa, Faustine Munishi, Upendo Nkone, Christina Shusho, Joshua Mlelwa
na Kwaya ya Wakorintho Wapili. Msama anaweka bayana kauli mbiu ya tamasha hilo ni Njooni wote tumsifu
Mungu kwa pamoja, tumuinue Mungu kwa nyimbo na kucheza mbele yake.