24.8 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani yamfilisi Mtanzania kinara dawa za kulevya

SHKUBANa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI ya Marekani juzi ilitangaza kutaifisha mali za bilionea Mtanzania, Ali Khatib Haji Hassan, maarufu Shikuba pamoja na mtandao wake wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya.

Shikuba ambaye ni mfanyabiashara maarufu Dar es Salaam, anamiliki msururu wa biashara kama vile maduka ya kubadili fedha (bureau de change), kampuni za ulinzi, majumba na utitiri wa magari ya kifahari.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha ya Marekani kupitia ofisi yake ya Udhibiti wa Mali Haramu za Raia wa Kigeni (OFAC), Shikuba na taasisi yake wameangukia katika sheria za nchi hiyo za kudhibiti mapapa wa unga wa kigeni (Kingpin Act).

Mbali ya sababu za kisheria, Marekani imesema bilionea huyo amekuwa akitumia faida haramu kutokana na biashara zake chafu kuhonga maofisa wa Serikali ya Tanzania ili asikamatwe na kushtakiwa.

“Bilionea Shikuba ni bwana unga mkubwa mwenye mtandao mpana kimataifa, husafirisha kimagendo shehena kubwa ya dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine kwenda Afrika, Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini kupitia makao yake Afrika Mashariki,” ilisema taarifa hiyo.

Kutokana na sababu hiyo, mali zote za Shikuba na taasisi zake zilizo ndani ya mipaka ya Marekani au ambazo ziko chini ya raia wa taifa hilo, zimetaifishwa huku raia wa Marekani wakionywa kuhusiana nazo.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa baada ya msako mkali wa miaka miwili, Shikuba alikamatwa mwaka 2014 na mamlaka za Tanzania kufuatia kuhusishwa na kilogramu 210 za heroin,  zilizokamatwa Januari 2012 mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa taarifa ya OFAC, Shikuba mara kwa mara amekuwa akiwahonga maofisa wa Serikali ya Tanzania ili kukwepa kukamatwa na kushtakiwa.

“Hatua ya leo (juzi) inaweka vikwazo kwa Ali Khatib Haji Hassan na mtandao wake haramu wa dawa za kulevya duniani. Mtandao huu hulenga kutumia faida haramu kuhonga maofisa wa Serikali za Afrika.

“Mapapa wa unga ikiwamo mtandao haramu wa Shikuba, hutishia mifumo ya fedha na hali ya utulivu wa kikanda, hivyo Wizara ya Fedha imebakia na dhamira yake ya kuendelea kuwafichua na kuwalenga wale wote wanaochochea biashara hii haramu ya dawa za kulevya duniani,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa OFAC, John E. Smith.

Shikuba hupata viwango vikubwa vya shehena za heroin kutoka vyanzo vilivyopo kusini magharibi mwa Asia na tani za cocaine kutoka kwa wasambazaji wa Amerika ya Kusini.

Kwa mujibu wa OFAC, Tangu mwaka 2006, Shikuba amekuwa akiagiza wafanyakazi wa mtandao wake kutuma shehena za heroin maeneo mbalimbali, ikiwamo China, Ulaya na Marekani.

Shikuba ni msambazaji mkuu wa wauzaji dawa za kulevya wa Tanzania, ambao mara kwa mara hupokea mamia ya kilogramu za heroin kutoka pwani ya Marekani, Pakistan na Iran.

Pia anasimamia mtandao mkubwa wa dawa za kulevya Amerika ya Kusini, ambao husambaza cocaine ya Amerika ya Kusini kuingia Afrika Mashariki kuelekea Ulaya na China.

Tangu Juni 2000, taasisi na watu zaidi ya 1,800 zimeguswa na sheria hiyo dhidi ya mapapa wa unga kwa ushiriki wao wa biashara ya kimataifa ya unga.

Adhabu kwa ukiukaji wa sheria hiyo huanzia faini ya hadi dola za Marekani milioni 1.075 kwa kila ukiukaji hadi adhabu kali ya makosa ya jinai.

 

ALIVYOKAMATWA DAR 2014

Baada ya kuzikimbia mamlaka mara kadhaa, Shikuba mwenye umri wa miaka 46, alikamatwa Februari 28, 2014 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam, baada ya msako mkali wa miaka miwili.

Shikuba anahesabiwa kama mmoja wa mapapa wa unga wenye nguvu na ushawishi zaidi Tanzania, akiwa amewekeza nguvu hadi serikalini kwa baadhi ya vigogo waliokuwa wakimlinda.

Kwa mara ya kwanza alipandishwa kizimbani Machi 13, 2014, akiunganishwa na watuhumiwa wengine, Maureen Liyumba ambaye ni binti wa Amatus Liyumba aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Othman Mohammed Nyamvi aliye maarufu kwa jina la Ismail Adam na Upendo Mohammed Cheusi ambaye kwa sasa ni marehemu.

Awali baada ya akina Liyumba kukamatwa na heroin yenye thamani ya Sh. bilioni 9.4 mkoani Lindi, walimtaja Shikuba ndipo polisi walipoanza kumfuatilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles