WASHINGTON, MAREKANI
WAHAMIAJI wanaoingia nchini Marekani kupitia mpaka wa Kusini, hawatapewa hifadhi tena chini ya sheria mpya ya uhamiaji, utawala wa Donald Trump umesema.
Taarifa iliyotolewa na idara ya haki na usalama wa kitaifa, inasema sheria hiyo mpya itakomesha visa vya wahamiaji waliyokiuka sheria kuingia Marekani.
“Rais ana uwezo wa kupiga marufuku wahamiaji kwa masilahi ya taifa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Suala la uhamiaji lilikuwa ajenda kuu ya kampeini ya Rais Trump katika uchaguzi wa mwaka 2018 katikati ya muhula.
Trump amekuwa akikabiliana na msafara wa maelfu ya wahamiaji kutoka Amerika ya Kati ambao wamekuwa wakitaka kuingia nchini Marekani kupitia mpaka wa Kaskazini.
Rais huyo ameamuru majeshi ya nchi hiyo kufanya doria katika mpaka huo kama hatua aliyosema ni ya kulinda nchi dhidi ya wahamiaji hao.
Kaimu mwanasheria mkuu, Matthew Whitaker na mkuu wa usalama wa kitaifa, Kirstjeb Nielsen, juzi walitangaza kile kinachojulikana kama sheria ya mpito.
Katika taarifa ya pamoja viongozi hao walisema rais ana mamlaka ya kufuatilia mbali uhamiaji wote endapo wahamiaji watakiuka vikwazo vinavyodhibiti shughuli zao.
Pia wanasema hilo linaweza kufanyika ikiwa uwepo wao nchini utahatarisha usalama wa Wamarekani.
Rais Trump anatarajiwa kuidhinisha agizo hilo kuwa sheria. Hatua hiyo imepingwa vikali na muungano unaotetea haki ya raia ukisema inakiuka sheria.
Maofisa wa muungano huo walisema: “Sheria za Marekani zinawaruhusu watu kuomba hifadhi wakiwa nchini mwao ama wakiwa katika kituo cha mpakani.”
Chini ya katiba ya Marekani, wahamiaji wana haki ya kusikilizwa hasa wanaposema wanahofia usalama wao katika taifa wanalotokea. Wale wanaotafuta hifadhi huwa watoroka nchini mwao kwa kuhofia maisha yao.
Chini ya sheria ya kimataifa watu hao wanatambuliwa kama wakimbizi.
Mhamiaji anayetafuta hifadhi ambaye sasa anasadikiwa kuwa nchini Marekani kwa njia haramu, pia anastahili kusikilizwa.
Juhudi zilizopita za utawala wa Trump kukabiliana na suala la wahamiaji zimekosolewa vikali kisiasa na kisheria.
Juni mwaka huu rais alitia saini amri ya utendaji kuahidi kuweka familia pamoja,” katika kituo cha kuwashikilia wahamiaji, baada ya wazazi na watoto kutenganishwa.
Siku kadhaa baadaye, mahakama ya juu zaidi ilidumisha marufuku ya usafiri iliyotolewa na utawala wa Trump dhidi ya mataifa kadhaa ya Kiislamu. Mwanzoni mahakama kadhaa ziliamua kwa hatua hiyo ilikiuka katiba ya Marekani.