BAMAKO, MALI
MARAIS wanne wa nchi za Afrika Magharibi wanatarajia kuelekea Bamako mji mkuu wa Mali kuanzia leo Alhamisi, Julai 23 kwa lengo la kusuluhisha mzozo wa kisiasa kati ya vuguvugu la M5 na Rais wa nchi hiyo Ibrahim Boubacar Keita.
Ujumbe huo wa ngazi ya juu wa Jumjuiya ya Kiuchumi ya Nchi za magharibi mwa Afrika (Ecowas) unaoundwa na Rais wa Niger Mahamadou Issoufou, Rais wa Senegal Macky Sall, Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo na Rais wa Cote d’Ivoire Alassane Ouattara, unatarajiwa kuelekea Bamako leo kwa lengo maalumu la kuzishawishi pande mbili zinazozona nchini humo kufikia mwafaka.
Wengi wanajiuliza iwapo watakuja na mapendekezo mapya, kinyume na yale yaliyotolewa na ujumbe wa hivi karibuni wa jumuiya hiyo likiwemo suala la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Hivi karibuni wapinzani nchini Mali walikataa pendekezo la Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za magharibi mwa Afrika Ecowas la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo kama njia ya kuhitimisha mgogoro unaoikabili nchi hiyo.
Awali, Rais Keita alikuwa ameafiki pendekezo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, kufanyiwa mabadiliko mahakama kuu na kuvunjwa bunge lakini wapinzani wamekuwa wakisisitiza kuwa mabadiliko hayo hayatoshi na wanamtaka aondoke madarakani.
Kuanzia Juni 10 Mali imekuwa ikishuhudiwa maandamano makubwa dhidi ya Rais Keita ambapo waandamanaji wanasisitiza kuwa lazima aondoke madarakani. Wapinzani wanasema rais huyo amefeli katika utendaji kazi wake kuhusu mgogoro wa muda mrefu wa waasi, mgogoro wa kiuchumi na mvutano ulioibuka baada ya uchaguzi wa bunge mwaka jana.
Wapinzani nchini Mali wameendelea kung’ang’ania msimamo wao wa kutaka kujiuzulu Rais wa nchi hiyo, Keita huku kukifanyika juhudi za kieneo na kimataifa za kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Viongozi wa upinzani nchini Mali chini ya mwavuli wa Harakati ya Juni 5 walisisitiza kuwa, Rais Keita anapaswa kujiuzulu, Bunge livunje na kisha kuundwe serikali ya muda.
Juzi wapinzani hao walikutana na ujumbe wa Jumuiya ya Ecowas kama moja ya juhudi za kutaka kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Wajumbe wa jumuiya hiyo ya kikanda walitoa mapendekezo kadhaa kwa upinzani hasa kujiunga na serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itaanzisha mageuzi ya kisiasa na mashtaka dhidi ya wahusika wa mauaji ya raia waliouawa wakati wa maandamano.
Hata kama upinzani nchini Mali unadai kwamba utatoa majibu yake rasmi kwa mapendekezo yaliyotolewa baada ya mkutano wao usiokuwa wa kawaida, lakini tayari baadhi yao wameonyesha kupinga mapendekezo hayo.
Mgogoro wa kisiasa nchini Mali ambao uliibuka baada ya kufanyika uchaguzi wa Bunge mnamo Machi mwaka huu, umezusha wasiwasi mkubwa si tu ndani ya nchi hiyo, bali pia katika nchi jirani na nchi hiyo.
Wiki iliyopita, Rais Keita alisema kuwa, anakaribisha hatua ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, kubadilisha wajumbe wa Mahakama Kuu na kulivunja Bunge. Hata hivyo wapinzani wake wamesema hatua hizo hazitoshi kwani wanachotaka wao na Rais Keita kuondoka madarakani.
AP