NA MWANDISHI WETU, MWANZA
SAKATA la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutangaza nia ya kuwania urais, limeibua mapya baada ya makatibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kudai walipewa mafuta lita 60 na posho.
Wakizungumza jijini Mwanza jana kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, baadhi ya makatibu hao walishangazwa na kauli ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo, kudai kuwa hakukuwa na kikao hicho cha siri.
Walisema Diallo akiwa mwenyekiti wa CCM, anapaswa kueleza ni nani aliyegharamia mafuta kiasi cha lita 60 walizopewa badala ya lita 20 walizozoea kupewa kwa wiki na chama na siyo kukanusha uwapo wa kikao hicho.
Alisema kwa ajili ya kikao hicho, baadhi ya makatibu wa CCM waliopo katika mkoa ambao Diallo yeye ni mwenyekiti, walielekezwa kuja Mwanza na magari yao kwa ahadi ya kupewa mafuta na posho ili kuhudhuria kikao hicho cha faragha.
“Tuliokuwapo katika kikao hicho ambacho mimi binafsi kilinipa wakati mgumu kutokana na baadhi ya wajumbe kuitwa kwa makundi kuzungumza na Pinda katika hema lililokuwa limeandaliwa Ikulu ndogo, tunajua anayesema hakipo alikuwapo.
“Ni siku ya historia kwangu kuona PM anang’atwa mbu, na sisi tuling’atwa sana na mbu, hatukuwa tukifahamu chochote, tulikuwa tukielezwa ‘waleteni watu fulani ni zamu yao’, baadaye tulipata taarifa kuwa kuna kampeni za siasa zilizokuwa zikifanywa katika mahema,” alisema katibu mmoja wa CCM ngazi ya mkoa.
Alisema mazungumzo hayo yalichukua muda mrefu kutokana na msimamo wa wajumbe toka Mkoa wa Mara, ambao walionyesha wazi kuwa walikuja na msimamo wao, hivyo kufanya vikao hivyo kwenda hadi usiku wa manane.