NA MWANDISHI WETU,
UHURU maana yake si tu kuondokana na mkoloni na lengo la Mapinduzi ya Zanzibar hayakuwa tu kumuondoa mkoloni, ni kuboresha maisha ya wananchi ili waone tofauti ya sasa na walivyokuwa.
Lakini pia Mapinduzi yenyewe kama tendo la kisiasa yalizalisha vidonda ambavyo hadi leo havijapona na vinahitaji kutibiwa. Nadhani kila tunapoadhimisha Mapinduzi ni lazima tukumbuke haya.
Hayati, Abeid Amani Karume, alijaribu kuonyesha kuwa uhuru maana yake ni kuwawezesha wananchi kudhibiti uchumi wao na hatimaye maisha yao. Na alionyesha kuwa Serikali ikiwa na nia inaweza kufanya maisha ya wananchi kuwa bora zaidi na hivyo kuutia aibu ukoloni na wakoloni wenyewe.
Kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanashika mashamba na ardhi na kuhakikisha kuwa kila Mzanzibari anaweza kwenda skuli na kupata huduma za jamii kama maji ya bomba na huduma za kiafya, Rais Karume alitaka kutuonyesha kuwa Serikali ya uhuru, ikidhibiti matumizi ya fedha na kuwa na viongozi wanaowapenda wananchi wenzao, hakuna linaloshindikana.
Tuliona kwa mfano, alijenga nyumba na kuwakabidhi wananchi, Pemba na Unguja, wakae bure, kwa gharama za ujenzi wa Serikali, ni ushahidi wa upendo aliokuwa nao kwa wananchi wenzake, lakini ilikuwa ni tendo lenye kuutia aibu ukoloni, kuwa miaka zaidi ya mia ya kututawala haikuweza kumpatia Mzanzibari hata mmoja kibanda, lakini yeye katika muda usiozidi miaka kumi ya Mapinduzi aliweza kuwajengea wananchi zaidi ya mia tano, nyumba bora na za kisasa za kuishi.
Zanzibar wakati huo lilikuwa ni taifa dogo, halikuwa na fedha nyingi, lakini Rais aliweza kutumia kilichokuwapo kuwaonyesha wananchi kuwa inawezekana kuboresha maisha ya wananchi. Viongozi waliomfuata hatujui kiliwatokea nini, maana yale majengo aliyoyaacha hayati Karume na kufariki dunia kabla ya kuyamalizia, yalikaa hivyo hivyo bila kumaliziwa kwa zaidi ya miaka arobaini hadi alipokuja Amani Abeid Karume, ndipo yakamaliziwa.
Kilishindikana nini baada ya kufariki Karume kumalizia na imewezekana tena vipi baada ya kuja kwa Rais Amani Karume.
Lakini tukiwa wakweli, hali ya uchumi wa wananchi siyo nzuri. Maisha bado ni ya gharama kwa wananchi na kwa maeneo yale ambayo watalii hutembelea maisha ni magumu zaidi kutokana na kupanda kwa gharama za kuishi. Hii inatokana na kupungua uzalishaji katika sekta kuu ya uchumi na kilimo kutotiliwa maanani. Uchumi wa Zanzibar una fursa nyingi sana katika kilimo, viwanda na utalii, lakini hazikuzwi.
Kwenye utalii, kwa mfano, kilimo kikiboreshwa utalii wa chakula ungewezekana na hivyo kuwavutia wananchi wengi kwenye chakula. Hili la utalii wa chakula unawezekana sana kwa mfano, katika mashamba yale ya spices- viungo, kungejengwa mfumo ambapo vyakula vya mapishi ya Kizanzibari vingetayarishwa katika hali ya usafi na watalii wangependa kuonja. Lakini uuzaji wa viungo vya chakula ndani na nje ya Afrika Mashariki ukitiliwa mkazo ungeweza pia kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi. Serikali ijenge programu ya maendeleo na kuisimamia na kuipatia fedha na wataalamu. Nina uhakika sekta ya kilimo inaweza kuboreka na wananchi kuwa na nafuu ya maisha.
Aidha, katika sekta hiyo ya utalii nilichokuta ni kuwa Serikali bado haiwezi kudhibiti mapato yake. Maeneo kadhaa yenye vivutio vya utalii hayajaboreshwa kwa kupatiwa huduma bora za kisasa kama vyoo na maji, maduka ya mahitaji maalumu na hata kuwahimiza wananchi kuanzisha maduka ya bidhaa za kitamaduni na hakuna mawasiliano ya simu na ulinzi pia.
Lakini pia ukusanyaji fedha hauko chini ya Serikali kuu katika baadhi ya vituo vya utalii. Utangazaji wa vivutio vya utalii Zanzibar bado ni wa hali ya chini sana na juhudi kubwa zinahitajika kwa kweli kama sekta hii itakuwa mwokozi wa uchumi wa Taifa na maisha ya wananchi visiwani humo. Vituo kama Ras Mkambuu, Chwaka na zaidi ya 28 vya Pemba ninavyovifahamu mimi kwa kweli havijulikani kwa Mtanzania ambaye hajafika huko na wengi wanaofanya utangazaji wa vivutio vya utalii ni wageni ambao huchagua vile vitu ambavyo wazungu huvipendelea na kuvitangaza.
Nimependelea kuzungumzia hali ya uchumi tu katika muktadha huu wa maadhimisho ya Mapinduzi kwa sababu nafahamu bila uchumi hakuna kinachowezekana katika nchi. Kwame Nkrumah alisema kuwa tuutafute kwanza uhuru wa kisiasa na mengine yote yatajaziwa, lakini pengine niongezee kuwa tuutafute kwanza ufalme wa kiuchumi na tutaona mengine yote yanajengewa kheri. Nchi kama haina uhuru na ukomavu wa kiuchumi, wananchi wake hawawezi kuwa huru na maadhamisho ya matukio ya kihistoria na kisiasa yanakuwa kwa ajili ya kuwafurahisha viongozi tu.
Na kujengeana matumaini ya uongo na viongozi kutoa hotuba ndefu ndefu za kuchonga tu, kulazimisha kuwa kuna maendeleo yamepatikana wakati kwa kweli ya Allah, ni watu wachache tu wanaonufaika. Yadumu Mapinduzi ya Zanzibar ilimradi yawe yenye mwelekeo ya kimaendeleo kwa faida ya wote!