25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAPATO TRA YAPAA

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kukusanya kodi ya Sh trilioni 3.65 katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2017/18.

Imesema makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 1.2 ikilinganishwa na   yaliyokusanywa katika mwaka wa fedha wa 2016/17.

Akitoa taarifa hiyo   Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema Julai mamlaka ilikusanya Sh trilioni 1.101, Agosti Sh trilioni 1.205 na Septemba Sh trilioni 1.345.

Katika robo ya kwanza ya 2016/17, TRA  ilikusanya Sh trilioni 3.60 na Julai ilikusanya   Sh trilioni 1.069 wakati  Agosti ilikusanya Sh trilioni 1.154 na Septemba Sh trilioni 1.378.

Kayombo alipuuza taarifa za baadhi ya watu waliokuwa wanasema makusanyo ya TRA yameshuka chini ya Sh trilioni moja kwa mwezi na kwamba ndiyo maana imekuwa haitangazi   tena mapato ya kila mwezi kama ilivyokuwa awali.

“Kuanzia mwaka 2015/16 mapato ya TRA hayajawahi kushuka chini ya Sh trilioni moja,na mafanikio hayo yametokana na mwamko mkubwa wa wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari.

“Mwamko wa wafanyabiashara kulipa kodi umechangia mafanikio makubwa ya TRA   kukusanya zaidi ya Sh trilioni moja.

“Tunaomba moyo huo wa uzalendo uendelee  tuiwezeshe serikali kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi,” alisema Kayombo.

Alisema TRA  inawataka wafanyabiashara kutoa risiti zinazotokana na mashine za  elektroniki(EFD) kwa kila mauzo ikiwa ni pamoja na kudai risiti kwa kila ununuzi ili kupata mauzo sahihi yatakayoiwezesha mamlaka kukokotoa kodi sahihi na kwa haki.

Kayombo alisema kila mwananchi anayenunua bidhaa anatakiwa kuhakiki risiti anayopewa na mfanyabiashara kama ni sahihi  na inaendana  na tarehe husika ikiwa ni pamoja na kiasi cha fedha alicholipa.

“Napenda kuwakumbusha wananchi wote kuhakiki risiti zao kabla ya kuondoka  kuona usahihi wa tarehe na kiasi cha fedha alicholipia bidhaa aliyonunua   kodi yake iweze kufika sehemu stahiki,” alisema Kayombo.

Kayombo pia aliwakumbusha wamiliki wa majengo nchini kulipia kodi ya majengo mapema kuepuka msongamano na usumbufu ifikapo mwishoni mwa mwaka wa fedha.

Alisema  wafanyabiashara wa michezo ya kubahatisha pia wanatakiwa kulipa kodi kwa mujibu wa Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Sura Namba 41.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles