28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MAPACHA WANAOFANANA HADI ALAMA ZA VIDOLE, ILA ASILI TOFAUTI

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI


WANAFAHAMIKA kama mapacha wa Dahms, wakiwa wamezaliwa kwa mfuatano huu Nicole, Erica na Jaclyn Desemba 12, 1977. Dahms ni jina la baba yao!

Wazazi wao lazima walishukuru kwa kubarikiwa wasichana wadogo watatu wazuri.

Watu pia walishangazwa upacha wao, shukrani zikiwa zaidi mwonekano wao mzuri wa nywele na macho ya bluu.

Uzuri wao, mwonekano mmoja, kufanya kila kitu pamoja kulitosha kuwafanya wajikusanyie mashabiki wengi tangu utotoni mwao katika mji wao mdogo.

Tangu wanazaliwa ilikuwa vigumu mno hadi kwa wazazi wao kuwatofautisha, kitu kilichowafanya wawawekee tattoo kila mmoja ikiwa na alama maalumu ya doa.

Nicole akiwa mzaliwa wa kwanza alikuwa na doa moja. Erica doa mbili na pacha wa mwisho Jaclyn hakuwekwa doa. Watatu hao huwezi kuwatenganisha popote pale na kuzidisha mkanganyko kwa marafiki na familia.

Walikulia Jordan, mji mdogo wa kule Minnesota na walisoma shule ya umma ya juu ya sekondari.

Kuishi katika mji mdogo kunamaanisha wepesi wa kufahamika katika jamii.

Watu wasiozidi 30,000 wanaishi Jordan wakati wasichana hao wakikua, kitu kilichomaanisha kila mtu aliwafahamu. Marafiki na mawakala wa urembo na mitindo waliweza kuwabaini mara moja kwa uzuri wao.

Wakati walipokuwa na umri wa miaka 16 tu waliweza kupamba ukurasa wa mbele wa jarida la mitindo kama washindi wakati wa tuzo ya vipaji vinavyoinukia.

Ukawa mwanzo wa kujikita kikamilifu katika tasnia ya mitindo na haikuchukua muda mrefu kabla ya kupamba moja ya majarida makubwa kabisa ya mitindo.

Wakati wakiwa wamefurahia kuonja uanamitindo, mapacha hawa wa Dahm hawakuwa wamepanga kuifanya iwe shughuli yao kuu.

Hivyo, wakajiunga Chuo Kikuu cha Minnesota, kusomea uuguzi wakiwa na matumaini kuwa siku moja wote watakuwa wauguzi tena katika hospitali moja.

Ni katika kampasi ya chuo hicho walikokutana na Jay McGraw, aliyekuja kuwa mume wa mmoja wao, ambaye ndiye chanzo cha kuwapo taarifa za kushtusha kuwahusu.

Dk. Phil, baba wa Jay McGraw ni mmoja wa watayarishaji watendaji wa kipindi maarufu cha televisheni kinachoitwa The Doctors.

Katika kipindi hicho, masuala mbalimbali ya kitabibu hujadiliwa na jopo la madaktari. Katika kila kipindi, wasanii au wanamichezo nyota hualikwa kuzungumzia masuala yao ya kitabibu na kutoa maoni na kuruhusu majadiliano.

Baada ya McGraw kumuoa Erica mwaka 2006, akawajiwa na wazo la kuwashirikisha mapacha hao watatu katika kipindi hicho, ambako wangezungumzia maisha yao na afya zao kama mapacha.

Umma ulipenda mno ujio wa wasichana hao kwa vile walivutia na kukanganya mno.

Erica, Jaclyn na Nicole wakawa wakionekana mara kwa mara katika kipindi hicho cha runinga, ambacho kwayo walizungumzia kila kitu kuanzia kupata mimba hadi mfanano wao kama mapacha.

Watayarishaji wa The Doctors mara wakapata wazo jipya; ambalo lingependekeza zaidi kipindi chao hicho cha TV.

Nalo likawa kupata mimba wakati mmoja na kweli ilitokea; baada ya kushika mimba wakati mmoja mwishoni mwa 2009 na mwanzoni mwa 2010.

Mapacha hao wakazaa wakati mmoja mwaka 2010. Si tu walizaa kwa wakati mmoja bali pia watoto wazuri wa kike.

Jay McGraw na watayarishaji wengine wa The Doctors walizidi kutafuta wazo, wakakutana na mapacha hao mwanzoni mwa 2017 wakiwa na ombi la kushangaza kwao.

Waliwataka waruhusu kumwingiza Mwandishi wa Jarida la Inside Edition, Lisa Guerrero, achunguze mfanano wao na asili ya mababu zao kupitia vinasaba (DNA) na sampuli ya mate.

Kwao na watazamaji wa kipindi hawakutarajia jambo la kushangaza, walikuwa na uhakika vipimo vitaoana. Yaani hakuna aliyetarajia kuwapo matokeo ya kushtusha.

Nchini humo vipimo vya DNA na asili ya watu vimejipatia umaarufu mkubwa, ambapo watu hulipa fedha kubaini kuhusu asili yao duniani, kampuni maarufu kwa kazi hiyo ikiwa pamoja na 23andMe.

Mapacha hao waliwasilisha sampuli zao za mate kwa kampuni hiyo wakasubiri matokeo. Hawakujua kabisa kuwa matokeo haya yataishtua dunia.

Matokeo yakaja, ijapokuwa hayakushangaza mapacha hao na watazamaji lakini yalionesha kuwa wao ni wamoja. Yaani wako sawa kila kitu.

Kwa mfano; Nicole anaweza kufungua sefu yenye alama ya vidole vya Erica kwa sababu alama zao za vidole zilikuwa karibu sawa. Yaani wote watatu wanaweza kuidanganya teknolojia ya alama ya vidole.

Jaribio la pili likawa kusaka mababu zao, yaani asili ya wanakotoka iwapo ni moja. Kama ilivyokuwa kwa DNA mapacha walitarajia jaribio la pili litatoa majibu sawa. Hata hivyo, haikuwa hivyo!

Vipimo vilionesha wakati wasichana wote watatu wakiwa asilimia 99 kutoka Ulaya walitofautiana utaifa.

Kwa mfano, Erica alikutwa kwa asilimia 16 asili taifa la Ireland na Uingereza huku Nicole akiwa na asilimia 2 zaidi Ireland na Uingereza. Imekuaje, matokeo hayo yalishangaza na kukanganya mapacha hao, madaktar na watazamaji wa kipindi hicho.

Matokeo zaidi yaliingia yakionesha tofauti kubwa zaidi ya asili ya mapacha hao. Vipimo vya The 23andMe vilionesha walikuwa na tofauti ya asili nyingine ya Ufaransa na Ujerumani; Nicole kwa asilimia 11, Jaclyn asilimia 18 na Erica asilimia 22.3.

Imekuaje mapacha wanaofanana vinasaba wakawa na asili tofauti? Lilikuwa swali lisilo na jibu.

Lilipokuja suala la nchi za Scandinavia walishtushwa kuona wakati Erica na Jaclyn wote wakiwa na asili moja-asilimia 7.4, alikuwa Nicole aliyekuwa na matokeo tofauti akiwa na asilimia 11.4 ya Scandinavia. Imekuaje, kila mtu alishtushwa.

Wote watatu hawakuweza kudhibiti mshtuko walioupata kwa vile walitokana na yai moja na wana DNA moja lakini asili mkanganyiko.

Dk. Travis Stork aliyealikwa katika kipindi hicho aliwatoa wasiwasi mapacha hao na watazamaji akisema kipimo kilichobainisha tofauti za asili hao hakipaswi kuchukuliwa uzitio kwa vile ni kawaida kuleta matokeo tofauti.

Mapacha hao kwa sasa wana watoto wa kiume baada ya awali kila mmoja kuzaa wa kike tena wote wakiwa wamezaliwa wakati mmoja. Na wote wanaishi na waume zao.

mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles